ZAIDI ya walimu 300 wa mkoani hapa, wanaweza kupoteza maisha kutokana na ugonjwa wa UKIMWI, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, baada ya kuongezeka maambukizi katika sekta hiyo.
Taarifa hiyo imetolewa na Katibu wa Chama cha Walimu (CWT), mkoani hapa, Abel Maruma, alipozungumza na Tanzania Daima mwishoni mwa wiki.
Alisema taarifa inaonyesha kuwa kila mwezi mwalimu mmoja hupoteza maisha, na kuwa wastani wa walimu 60 hufa kila mwaka kutokana na ugonjwa huo.
Katibu huyo alisema, kutokana na kasi hiyo ya maambukizi, chama hakiwezi kupuuza hali hiyo ambayo inapunguza nguvu kazi ya walimu, kwani serikali imekuwa ikiwaandaa walimu na kuwaajiri kila mwaka, ili kujaza mapengo hayo.
Maruma aliongeza kuwa, kila mara chama hicho kinawakutanisha wanachama wake ili kuzungumzia namna ya kuchukua tahadhari ili kuepukana na maambukizi hayo.
Aliwataka walimu hao wapime afya zao ili kuelewa hali halisi, na kuishi kwa matumaini kwa muda mrefu na kuendelea kulea familia zao.
Akizungumzia mafanikio mbali mbali yaliyopatikana tangu chama hicho kianzishwe, Maruma alisema chama hicho kimefanikiwa kujenga jengo la ghorofa 10 lenye thamani ya sh bilioni 5.6 jijini Dar es Salaam.
Alisema jengo hilo lililojengwa jijini Dar es Salaam, linatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete.
Aidha, alisema juhudi hizo pia zinaendelezwa kwenye mkoa na wilaya, ambapo kwa upande wa Wilaya ya Kongwa, wanachama wa chama hicho wanatarajia kujenga jengo la ofisi ya chama hicho.
Maruma alisema lengo la chama hicho ni kuendelea kuongeza wanachama wengi zaidi ya waliopo sasa wanaofikia 6,519 kutoka katika matawi 155 ya chama hicho yaliyopo mkoani hapa.
Katibu huyo wa CWT alikuwa akizungumza kwenye kilele cha sherehe za Siku ya Mwalimu Duniani zilizoadhimishwa kimkoa wilayani Kongwa.