MHADHIRI Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengondo Mvungi, amemshauri, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Balali, kuwaeleza ukweli Watanzania, kuhusu hali ya uchumi wa nchi na si siasa.
Akizungumza na Tanzania Daima, kwenye mahojiano maalumu jana jijini Dar es Salaam, Dk. Mvungi alisema aliyoyaeleza Balali, si ya kweli kuhusu hali ya uchumi hapa nchini.
Dk. Mvungi alisema anaposema kuwa hali ya uchumi si mbaya ilhali bei ya bidhaa kama saruji iliyokuwa ikiuzwa sh 8,000 na sasa sh 11,000, lori la mchanga sh 60,000 sasa sh 150,000 si ya kupuuza.
Alisema bei ya chakula kama mchele ulikuwa ukiuzwa kilo sh 450 hadi 550, sasa unauzwa kati ya sh 1,000 hadi 1,500 kwa kilo, na bei ya shambani ambayo ilitegemewa kuwa rahisi, sasa unauzwa sh 600 hadi sh 700 kwa kilo moja.
Alisema mwaka jana bei ya lita moja ya dizeli ilikuwa sh 930, sasa hivi lita moja ni sh 1,240, na kuwa katika hali kama hiyo huwezi kuthubutu kusema uchumi wa nchi haujayumba.
Mhadhiri huyo alisema bei ya bidhaa na huduma nyingine zimepanda mara mbili na nyingine tatu, na thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani imeshuka kutoka sh 930 kwa dola Desemba 2005, hadi kufikia sh 1,275 hivi sasa.
“Kwa hiyo Balali, alivyosema uchumi haujayumba, hayumkini hazungumzii uchumi wa taifa letu, atuambie anazungumzia uchumi wa nchi gani na atueleze ni jinsi gani kipato cha Mtanzania kimekua mara tatu ili kumudu ongezeko hili la bei.
“Balali, aonyeshe pia kwa kigezo cha uzalishaji ni jinsi gani uzalishaji wa mali umekua kwa miezi sita iliyopita licha ya kuwa na tatizo la umeme hadi hivi sasa.
Alisema anachokieleza Balali ni siasa ambazo kwa yeye kama mtaalamu hazimfai, kinachomfaa ni kueleza ukweli wa kiuchumi.
Mhadhiri huyo alisema Watanzania wa sasa wengi ni wasomi na wenye uelewa kwenye mambo mengi ya kiuchumi na kisiasa, na hapaswi kuambiwa uongo au porojo za kisiasa.
Wiki iliyopita Gavana wa Benki Kuu, Balali, aliwaambia waandishi wa habari kuwa uchumi wa nchi haujayumba na thamani ya shilingi bado ni imara