Na Waandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amewaeleza viongozi wa serikali ya Burundi na wale wa kikundi cha waasi cha Palipehutu-FNL kufikia muafaka, kwani amani ya watu wa Burundi iko mikononi mwao.
Rais Kikwete alisema hayo jana alipokuwa akifungua mkutano wa mazungumzo ya amani ya Burundi kati ya serikali na kikundi cha waasi cha Palipehutu-FNL uliofanyika kwenye hoteli ya Kilimanjaro Kempinsk.
Alisema kuwa uamuzi wa kumaliza mapigano na kuleta amani ya Burundi uko kwenye himaya ya viongozi hao na aliwapongeza kwa uamuzi wao wa kurejea tena kwenye meza ya mazungumzo kuhusu amani ya nchi yao.
Rais Kikwete alisema kuwa hakuna mtu wa nje wa kuamua kuhusu amani ya Burundi na kwamba uamuzi ni wao kama wataamua kuheshimu juhudi za marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais mstaafu wa Afrika Kusini Nelson Mandela.
Alisema Tanzania inaelewa matatizo yanayowapata watu wa Burundi kwa kuwa ni miaka 40 sasa Tanzania imekuwa mwenyeji wa wakimbizi kutoka Burundi.
Rais Kikwete alisema Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za upatikanaji wa amani na aliuomba Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, washiriki wa upatikanaji wa amani katika ukanda wa nchi za Maziwa Makuu na jumuia za kimataifa kusaidia kuleta matumaini kwa watu wa Burundi.
Naye mwenyekiti wa jitihada za kuleta amani katika Ukanda wa nchi za Maziwa Makuu, Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameonya kuwa mazungumzo hayo yasivunjike kama yale ya mwanzo.
Rais Museveni ambaye ujumbe wake ulisomwa kwa niaba yake na Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Ibrahim Mukiibi, alisema kuwa muda mwingi umepotea tangu mazungumzo ya awali yavunjike mwaka jana na kwamba ni muhimu mazungumzo ya sasa yakafikia mwisho.
Naye kiongozi wa kikundi cha Palipehutu-FNL, Agathon Rwasa aliishutumu serikali ya Burundi kwamba imekuwa ikishambulia watu wake na kuleta uhasama kwa wananchi.
Rwasa aliwaeleza waandishi wa habari nje ya ukumbi wa mikutano kuwa Mei 15, 2005 walitia saini mkataba wa kusimamisha mapigano, lakini waliporudi Burundi majeshi ya serikali yalianzisha chokochoko kwa kuwashambulia watu wao.
Alitaka jeshi na polisi wa Burundi wabadilishwe na wananchi wapewe uhuru wa kutoa maoni yao ambao alidai uhuru huo haupo na nchi imegubikwa na ukabila.
Rwasa alisema kuwa mgogoro wa Burundi hauwezi kumalizika kwa kugawana vyeo, kwanza inatakiwa kuondoa uhasama wa kikabila ulioota mizizi kuanzia kwa wananchi wenyewe.
Alizitaka jumuia ya kimataifa kuingilia kati vurugu zinazofanywa na jeshi la Burundi na kushinikiza mabadiliko katika jeshi hilo.
Naye Waziri wa Usalama wa serikali ya Burundi, Evarist Ndayishumiya akiongea na waandishi wa habari alisema kuwa haiwezekani kubadili jeshi au polisi kama kinavyodai kikundi cha FNL.
Alisema kuwa serikali ya Burundi inafuata katiba na kwamba kikundi hicho kinatakiwa kuingia katika serikali ili kutekeleza katiba ya Burundi.
Ndayishumiya alisema kwamba kikundi cha FNL kimekuwa kikishambulia watu na ndiyo maana jeshi limekuwa likipambana nao.
Alisema mkutano wao huo ndiyo wanategemea kupata jibu la matatizo hayo na kuleta amani ya Burundi kwa kuwa wananchi wanawategemea wao.
Baadaye akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa mkutano, mpatanishi wa mkutano huo wa amani, Waziri wa Ulinzi na Usalama wa Afrika Kusini, Charles Ngakula, alisema kuwa jinsi mazungumzo yalivyoenda jana, kuna dalili za mkutano kukamilika kwa amani.
Alisema,mkutano wa jana ni sehemu ya maandalizi ya mkutano kamili wa ajenda hiyo ya amani ya Burundi utakaofanyika wiki ijayo.
Kutoka gazeti la Uhuru