Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Seif alalamika kunyang’anywa ulinzi
Seif alalamika kunyang’anywa ulinzi
By Habari Tanzania | Published  10/30/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imemnyang’anya ulinzi tangu kumalizika Uchaguzi Mkuu, Oktoba mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema kumnyang’anya ulinzi kunampa wasiwasi, hasa wakati huu ambao kuna matukio mengi ya uhalifu wa kutumia silaha.

Alisema baada ya askari kutoonekana nyumbani kwake, alijaribu kuulizia sababu ya kutofika, lakini mpaka sasa hajapata maelezo yoyote ingawa ni haki yake kikatiba kulindwa.

Alisema ni yeye pekee ambaye amenyimwa ulinzi lakini, mawaziri viongozi wastaafu wenzake, Ramadhan Haji Faki na Dk. Mohammed Gharib Bilal wanapatiwa ulinzi kama kawaida.

Maalim Seif alisema kuwa mlinzi wake kutoka Idara ya Usalama wa Taifa amekuwa akifanya kazi ya kumlinda anapokuwa Zanzibar pekee na si nje ya Zanzibar kwa sababu idara yake haimpi fedha za safari za nje ya Zanzibar.

Alisema kitendo hicho kinamnyima haki yake ya kikatiba kwa vile anapaswa kulindwa akiwa ndani na nje ya nchi.

Maalim Seif alisema kwamba pia kumekuwapo na urasimu wa kucheleweshwa mafao yake anayopaswa kulipwa kila mwezi, na wasaidizi wake hulazimika kwenda Idara ya Hazina mara kwa mara kufuatilia.

Alisema pamoja na kuwa ana akaunti za benki, lakini idara hiyo inaendelea na utaratibu wa zamani wa kumtuma mjumbe kumletea fedha zake mkononi.

Alisema mapema mwaka huu alitaka kwenda nje ya nchi kuangaliwa afya yake, lakini aliambiwa kuwa hakuna fedha, wakati ni haki yake kusafiri kila mwaka kwa gharama za serikali kama kiongozi mstaafu.

Maalim Seif alisema alipokuwa kiongozi kwenye Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), alifanya kazi kwa uadilifu, hivyo anapaswa kuheshimiwa.

Akijibu baadhi ya lawama hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Bakar Khatib Shaaban, alisema Maalim Seif kama anahisi hatendewi haki, alipaswa kwenda kulalamika kwa Kamishna wa Polisi Zanzibar, Khalid Idd Nuizan.

Alisema yeye hawezi kusema chochote kwanini itifaki ya viongozi wastaafu inamtenga kwa vile msemaji wa suala hilo ni Kamishna mwenyewe.

“Mimi nilifikiri unaniuliza suala la msingi, kumbe ni kuhusiana na suala hilo, naomba umuulize Kamishna,” alisema Bakar.

Akizungumzia madai ya Maalim Seif kutolipwa baadhi ya mafao yake, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi, Khamis Mussa alisema tangu kuteuliwa kushika wadhifa huo, hajapata barua ya malalamiko ya Maalim Seif kudai mafao yake ya nyuma.

“Kwa upande wangu, nafahamu wastaafu wote wanalipwa kila mwezi, lakini kuhusu madeni yake ya nyuma, sijaona malalamiko yake kwa maandishi na siwezi kuzungumza hilo kupitia vyombo vya habari,” alisema Mussa.

Maalim Seif aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM na SMZ, ikiwamo Mkuu wa Idara ya Mipango ya CCM na Waziri Kiongozi Zanzibar


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.