Baadhi ya Watanzania ambao wanatuhumiwa kula njama za kuiba mali ya mamilioni huko Marekani, inasemekana kama si matatuzi dili hilo huenda lisingebainika.
Taarifa zilizosambazwa kwenye mtandao na kuyafikia magazeti nchini zinadai kuwa watuhumiwa hao baada ya kunyaka mamilioni hayo walianza kutumia fedha katika starehe mbalimbali kabla ya vyombo vya sheria kuwakamata.
Jambo hilo limefahamika wakati kesi yao inapamba moto.
Ujumbe mbalimbali wa Internet ambao umeyafikia magazeti hapa nchini unadai kuwa Watanzania hao walikuwa wakimwaga maraha na starehe mbalimbali katika mitaaa ya miji mbalimbali ya Marekani.
Kana kwamba hiyo haitoshi, ujumbe huo unasema watu hao walikuwa wakionekana kwenye magari ya kifahari ikiwa ni pamoja na magari ya kisasa aina ya Ranger Rover, Mercedes Benz, BMW na Hummer.
Mmoja wa watuhumiwa hao inadaiwa alikuwa na magari matatu ya kifahari na ya bei mbaya, ambapo kila gari lilikuwa na thamani ya dola 80,000 ambazo ni karibu shilingi milioni 100 za Tanzania.
Mtu huyo anasemekana alilinunua gari hilo kwa kulipa pesa taslimu.
Wengi wa watuhumiwa waliokamatwsa walikuwa wakiishi katika eneo la Houston, sehemu ambayo ni jimbo la Texas la Marekani.
Habari zaidi zinasema watu hao walikuwa wanapenda kuvaa nguo za gharama na za kisasa wakiwa wanatumia fedha nyingi katika vilabu vya usiku ambavyo hutembelewa sana na Watanzania wanaoishi nchini Marekani.
Pia watu hao wanasemekana walikuwa ni watumiaji wazuri wa vinywaji vya gharama kubwa kama vile ’champagne’ ikiwa ni pamoja na kuandaa hafla (karamu) mbalimbali za vyakula na vyinywaji.
Watuhumi hao kwa pamoja wanadaiwa kula njama za kuiba vifaa vya mamilioni ya dola kutoka kampuni maarufu ya vifaa vya kompyuta na mawasiliano ya elektroniki Hewlett-Packard (HP) nchini Marekani.
Sita walifikishwa kortini wiki iliyopita ambako hata hivyo walikana shtaka.
Watu hao walidakwa na shirika la upelelezi la Marekani la FBI baada ya upelelezi wa muda mrefu.
Waliofikishwa kortini ni Njaidi Othman Njaidi,35,Wasia Kesi Maya,28,Abby Hussein Omar,24,Ahmed Juma Khalid,30, Frederick Omondi, 31, na James Hill ,25.
Wengine watatu Franklin Lauwo,35 na Misso Canute Temu,30, inaaminika walirejea nchini wakati James Mtae, 27 , inaaminika bado yupo Houston au Dallas.