Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kikwete awageukia wanaharakati wa Kiislamu
Kikwete awageukia wanaharakati wa Kiislamu
By Habari Tanzania | Published  10/29/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:

Na Waandishi Wetu

UAMUZI wa viongozi wa ngazi za juu wa serikali na kidini, wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete, kuvamia ngome kuu za makundi ya kidini yenye nguvu na ushawishi mkubwa katika jamii umeonekana kuwa mkakati wa makusudi wa kudhoofisha nguvu za makundi hayo na kuleta utangamano, uchunguzi unaonyesha.

Kwanza uamuzi wa Kikwete kuswali katika msikiti wa Kwa Mtoro, ambao ndiyo ulikuwa ukiaminika kuwa ngome ya Waislamu wenye msimamo mkali, unaonekana dhahiri kuvunja nguvu za wanaharakati hao wa Kiislamu katika kudai yale wanayoamini kuwa wamekuwa wakinyimwa na serikali za Chama Cha Mapinduzi (CCM).Pamoja na kuwa vuguvugu la harakati linaonekana kuzimika katika msikiti huo katika miaka ya hivi karibuni, lakini mwelekeo wa viongozi hao wa kukabiliana nao umeonekana kuwa ni juhudi za kujaribu kushirikiana nao zaidi kabla vuguvugu llilopoa halijaibuka tena.

Ingawa katika miaka ya mwanzo ya akiwa madarakani Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi alikuwa akiswali mara kwa mara katika msikiti huo wakati wa uhai wa aliyekuwa Imamu Mkuu wa msikiti huo, marehemu Sheikh Kassim bin Jumaa, lakini kipindi hicho haukuwa na harakati za kudai haki za Waislamu kama ilivyokuja kutokea baadaye.Hata hivyo, Mwinyi hakukanyaga tena katika msikiti huo hadi alipoondoka madarakani baada ya harakati hizo kuanzishwa mskitini hapo, hatua iliyotafsiriwa kama ilikuwa kukwepa kuhusishwa na vuguvugu la harakati hizo.Uamuzi huo wa Rais Kikwete umeonyesha nia ya kuzika makundi ambayo yamekuwa ni moja ya udhaifu wa serikali karibia zote kuanzia ile ya awamu ya kwanza, kiasi cha kusababisha wakati mwingine nguvu nyingi kutumika kukabiliana na makundi hayo.

Kabla ya hatua hiyo ya Rais, Makamu wa Rais, Dk Ali Mohammed Shein, alipata kuswali na kushiriki katika mashindano ya kusoma Kurani na kutunukiwa tuzo ya ushiriki, hatua ambayo haikuwahi kufanyika hapo kabla.Kama haitoshi, Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Issa bin Shaaban Simba, pia aliwahi kuswali katika msikiti huo miezi michache kabla ya kuingia mwezi mtukufu wa Ramadhan, lengo likijionyesha kuwa ni kama linalofanana na waliomfuata baadaye yaani, Rais Kikwete na Dk Shein.Katibu wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, aliielezea dhana hiyo kwa mitizamo miwili. Wa Kiislamu na wake (Ponda) binafsi.

Kwa upande wa mtazamo wa Kiislamu, alisema iwapo viongozi hao walikwenda katika nyumba ya ibada ya Kiislamu kama viongozi wa serikali, dhana kama hiyo inaweza kujengeka na kuibua maswali kutokana na ujumbe watakaokuwa wamekwenda nao katika nyumba hiyo ya ibada.“Kama walikwenda kama Waislamu, Uislamu hauna mipaka kwa watu wa taasisi, shirika, jinsia au kabila moja kuingia kwa wakati mmoja au zaidi katika nyumba ya ibada za Waislamu, isipokuwa kama kuna kitu kitajitokeza katika ujumbe watakaoutoa katika nyumba ya ibada,” alisema Sheikh Ponda.

Kwa mtazamo wake binafsi, aliwashauri viongozi hao kwamba, kama Waislamu, wanapokwenda katika nyumba za ibada, wanatakiwa wawe na kitu cha ziada kitakachowasaidia Waislamu wenzao kama inavyofanywa na viongozi wenzao Wakristo wanapokwenda makanisani.Naibu Imamu Mkuu wa Msikiti wa Kwa Mtoro, Sheikh Khalifa Khamisi, alisema kwa miaka mingi imekuwa ni jambo la kawaida kwa viongozi wa serikali Waislamu kushiriki ibada katika msikiti huo kwa kuwa ni haki yao kama Waislamu kufanya hivyo msikitini hapo.

“Rais ni Muislamu, ana haki na hatukumwalika ila tuliposikia anakuja kuswali Idd katika msikiti wetu, tulifarijika sana na akaja, mambo haya ni ya kawaida na ni uamuzi wa Rais mwenyewe kuamua msikiti gani akaswali,” alisema Sheikh Khalifa ambaye pia ni Mdhamini na Katibu wa Bodi ya Wadhamini wa msikiti huo.

Hata hivyo, alisema ushiriki wa Dk Shein katika mashindano ya kusoma Kurani ambayo yamekuwa yakiandaliwa na msikiti huo kwa miaka mingi hususan katika mwezi mtukufu wa Ramadhan, ulitokana na kualikwa na uongozi wa msikiti kwenda kufungua mashindano hayo.Kuhusu Mufti Simba, alisema naye pia aliswali msikitini hapo kwa kualikwa na uongozi wa msikiti baada ya (Mufti) kuridhika na taarifa za uuzwaji wa kiwanja cha Waislamu cha Chang’ombe, Temeke alizopewa na uongozi wa msikiti huo.

Hata hivyo, wakati dhana hiyo ikipewa umuhimu wa kipekee, uchunguzi wa Mwananchi Jumapili unaonyesha kuwa, kasi na ukali wa harakati za Kiislamu katika msikiti huo, vilianza kupungua kwa kiasi kikubwa wiki chache baada ya marehemu Sheikh Kassim bin Jumaa kutoka rumande katikati ya mwaka 1993.Hali hiyo ilishamiri siku chache kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 na baada ya uchaguzi huo kufanyika ambapo sehemu kubwa ya wanaharakati hao waliamua kuuhama msikiti huo na kwenda kuendeleza harakati hizo hadi sasa katika misikiti mikuu ya harakati iliyoko ukiwamo msikiti wa Mwembechai, Mtambani, Taqwa (Mwananyamala), Mwenge na Temeke Tungi.

Hatua ya kuswali katika msikiti huo na kisha mara kadhaa kuwafuturisha viongozi wa ngazi za juu wa dini zote Bara na Zanzibar ni ishara nyingine, inayoonyesha mkakati huo umelenga kukomesha kama si kuzika kabisa tofauti za kidini miongoni mwa dini.Mkakati huu mpya wa Rais, hapana shaka unayaweka makundi hayo yaliyopo katika mapambano ya kudai wanachofikiri wao ni haki yao kwenye njia panda na kwa upande mwingine kuonyesha nuru ya matumiani ya mshikamano.

Utaratibu huu wa Kikwete hata kama alisema kwamba ataendeleza yaliyoanzishwa na awamu ya tatu, ni dhahiri anataka kufanya mabadiliko makubwa ya kimfumo na utekelezaji wa majukumu kiasi kwamba Watanzania katika makundi yote wajihisi zaidi wamoja.Akihutubia Baraza la Eid el Fitr lililofanyika Jijini Arusha mwanzoni mwa wiki hii, Rais Kikwete alisema watu wa imani tofauti katika jamii wataendelea kuwepo, hivyo kila mtu lazima aukubali ukweli huo na akubali kuishi na mwenzake wa dini na dhehebu tofauti.

"Hili linawezekana kwani ndiyo ilivyo hivi sasa hapa kwetu," alisema Rais Kikwete na kusisitiza kuwa serikali anayoiongoza, haitarudi nyuma katika kuheshimu uhuru wa raia wa kuabudu na kuhubiri dini bila kuchochea chuki na uhasama miongoni mwa wafuasi wa madhehebu na dini nyingine.Alisema yeye na wenzake serikalini, watakuwa wakali na wepesi wa kuchukua hatua kuhakikisha watu wachache wakorofi hawavurugi nchi kwa kuchochea uhasama na kutokuelewana kati ya Waislamu na Wakristo.

Muhibu Said na Yahya Charahani


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.