Na Khamis Hamad
MAANDALIZI ya Tamasha la Uhuru yamepamba moto, na Halmashauri ya Biashara ya Nje (BET) imewaomba wadau mbali mbali kushiriki katika kulifanikisha.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa BET, Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Edwin Rutageruka, alisema kwa vile litakuwa la kwanza kufanyika hapa nchini tokea uhuru, ni vema wadau kutoka sekta zote wakaungana na halmashauri hiyo kuhakikisha linafanikiwa kama lilivyokusudiwa.
Mkutano huo uliofanyika jana, ulilenga kutoa tathmini ya mafanikio ya maandalizi ya tamasha hilo, ambapo Ruta alisema taarifa za kuandaliwa kwake tayari zimefikishwa kwa Watanzania wote, baada ya timu zilizoundwa kutembelea mikoa yote na kuwaelimisha wananchi.
Tamasha hilo ambalo litafanyika kwenye Viwanja Vya Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa, Dar es Salaam kuanzia Desemba mbili hadi 23 mwaka huu, limeandaliwa na BET kwa lengo la kuhamasisha maendeleo ya uchumi kwa kutumia biashara.
Malengo mengine ni kuwakutanisha wafanyabiashara wa wadogo na wakati ili waweze kufahamiana na kisha kuweka mtandao wa pamoja wa kibiashara na hivyo kukuza mauzo ya bidhaa zao kwenye masoko ya ndani na nje.
Alisema, sambamba na wafanyabiashara, tamasha hilo litawanufaisha wananchi wa kawaida kutokana na kuwa litatoa fursa kujionea vivutio mbalimbali, ukiwemo muziki wa dansi, ngoma za asili na bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na zile zitokazo nje.
Kutokana na manufaa hayo kwa jamii, BET imewaomba wadau wake ambao ni wafanyabiashara, watu binafsi na taasisi nyingine kujitokea kuchangia gharama mbalimbali ili kusaidia kufanikisha tamasha hilo.
Kwa mujibu wa Rutageruka, wadau hao wanaombwa kuchangiagharama za matangazo ya tamasha hilo kwenye vyombo vya habari, michezo na burudani, mashindano ya michezo kama vile mbio za mbuzi na uchapishaji wa majarida.
“Sherehe za uhuru wa nchi yetu zinapaswa kuenziwa kwa kuwa na shamrashamra ili kuwawezesha wananchi waweze kusherehekea na familia zao, kwahivyo tunakusudia kulitumia tamasha hilo la Uhuru kuwa kampeni ya ‘nunua bidhaa za Tanzania, jenga Tanzania,” alisema.