Na Mwandishi Wetu
KIONGOZI maarufu wa dini ya Kiislamu nchini, Sheikh Yahya Hussein, amesifu hotuba ya Rais Kikwete aliyoita mjini Arusha kwenye Baraza la Idd, kwamba imetoa ukweli kuhusu ufujaji mali uliokuwa ukilikumba Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
“Ilikuwa ni hotuba ya mwaka, yenye ukweli mtupu na uwazi, kwani ni ya kuisaidia BAKWATA ipate uhai mpya, sababu hivi sasa Waislamu ambao wameitelekeza, walikuwa wanaamini BAKWATA ni wezi wa mali za Waislamu,” alisema Sheikh Yahya.
Sheikh Yahya aliwaambia waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), majengo na kashfa za kuuzwa baadhi ya viwanja vya BAKWATA hali iliyosababisha kufukuzwa kwa baadhi ya viongozi ni sehemu ya ufujaji huo.
Huku akionyesha baadhi ya nyaraka za mawasiliano baina ya serikali na baraza hilo, aliongeza kuwa kutaifishwa kwa mali hizo baada ya Azimio la Arusha, kulitokana na kukosekana kwa ufuatiliaji makini wa mali za baraza.
Hata hivyo, Sheikh Yahya alisema kuwa hajui, hatma ya ufuatiliaji wa fidia hiyo, kwani jukumu alilopewa na aliyekuwa Mufti wakati huo mwaka 1997 ya kufuatilia mali za BAKWATA hanalo tena.
Juu ya nini kifanyike, Sheikh Yahya alisema: “Nashauri mali zote za Waislamu zilizo chini ya BAKWATA zirudisahwe serikalini, BAKWATA na jumuiya nyingine za Waislamu zitoe mdhamini mmoja mmoja katika kuangalia mali hizo.”
Katika hotuba aliyoitoa mjini Arusha, Rais Kikwete alielezea kusikitishwa na vitendo vya ufujaji ndani ya Baraza, hali iliyosababisha hata baadhi ya wafadhili kutokuwa na imani na viongozi waliokuwa madarakani na aliitaka kuwa na sera na mwongozo sahihi wa shughuli zake .