Na Ester Bulaya
RAIA wa Uingereza Nicholaus Mason (53) anayekabiliwa na mashitaka ya wizi wa sh. milioni 82.5 (dola za Marekani 65,000) jana aliangua kilio katika Mahakama ya Kisutu Dar es salaam baada ya kukosa wadhamini.
Mason alimwaga machozi hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi Sivangirwa Mwangesi, anayesikiliza kesi hiyo.
Mshitakiwa huyo ambaye ni Mkurugenzi wa Mradi wa Maendeleo Handeni mkoani Tanga ,alifikishwa mahakamani hapo juzi na kusomewa shitaka na mwendesha mashitaka, Charles Kenyela, ambapo jana alifikishwa kwa ajili ya kudhaminiwa lakini wadhamini hawakutokea.
Sababu iliyomtoa machozi raia huyo wa Uingereza, ni pale askari alipoita wadhamini kwa ajili ya kumdhamini mshitakiwa huyo lakini hakukuwa na mtu aliyejitokeza na kumfanya aangue kilio huku akijikuna kichwa na kufikicha macho kwa kuhofia kwenda tena rumande.
Mason aliyetinga kizimbani huku akiwa ameshika mfuko mdogo mweupe wa ‘rambo’ alionekana kuchanganyikiwa aliposikia wadhamini wake hawaonekani, kitendo kilichosababisha kutotulia kizimbani na kupapasa macho huku na kule na kuendelea kujiinamia akiwa amesimama na kuuma vidole kwa kutoamini kilichotokea.
Akihairisha kesi hiyo baada ya wadhamini kutotokea, Hakimu Mwangesi alisema: “Sasa ndugu yangu hauna wadhanimi ukafurahie kuishi Segerea hasa weekend hii, mpaka Novemba 8, mwaka huu, ukipata wadhamini uje Jumatatu.”
Mason katika shitaka la kwanza anadaiwa Septemba 12, mwaka jana katika benki ya Standard Chartered tawi la NIC Life House, Dar es Salaam aliiba sh. 50,800,000 (dola 40,000).
Katika shitaka la pili Septemba 21, mwaka jana katika benki hiyo aliiba sh. 31, 750,000 (dola 25,000), inadaiwa fedha hizo alizipata kupitia kampuni ya maendeleo vijijini kwa ajili ya maendeleo ya watu wa vijiji kadhaa, ambapo alizitumia kwa matumizi yake badala ya maendeleo ya vijiji hivyo.
Mshitakiwa huyo ameshindwa kutimiza mashariti ya dhamana kwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaotia saini dhamana ya sh. milioni 10 kila mmoja.