Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mama Salma mwenyekiti wa taasisi mpya
Mama Salma mwenyekiti wa taasisi mpya
By Habari Tanzania | Published  10/28/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
Itasaidia elimu ya wasichana, matatizo ya wanawake
 
Na Njumai Ngota
 
TAASISI ya Kijamii ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) imetenga sh. milioni 230 kwa ajili ya kusomesha watoto watano wa kike kila mkoa Tanzania Bara wanaotoka katika familia masikini na watoto yatima kuanzia mwakani.
 
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete, ambaye ni mke wa Rais Jakaya Kikwete, wakati wa uzinduzi wa taasisi hiyo uliofanyika katika viwanja vya ofisi ya WAMA, mtaa wa Luthuli, Dar es Salaam.
 
Akifafanua kuhusiana na fedha hizo, alisema sh. milioni 200 zimetengwa kwa ajili ya watoto watano kutoka kila mkoa kwa upande wa Tanzania Bara watakaochanguliwa kujiunga na sekondari kuanzia mwakani.
 
“Watoto hao watakuwa ni wanaotoka katika familia masikini na yatima wasiokuwa na walezi,” alisema.
 
Aliongeza kwamba wanafunzi wengine 20 wa kike watakaochanguliwa kujiunga na Chuo Kikuu WAMA itawasaidia kuwapatia mahitaji muhimu, zikiwa zimetengwa sh. milioni 30 kuwasaidia katika miaka mitano watakayokuwa chuoni.
 
Pia WAMA itachangia sh. milioni 25 kwa Chama cha Wanawake Madaktari (MEWATA) kwa ajili ya uchunguzi wa kansa ya matiti kwa wanawake 1,000, zikiwa ni gharama za upimaji.
 
Mama Salma alisema wameamua kuanzisha WAMA kutokana na kukereketwa na hali ya wanawake nchini na dhamira ya kutaka kutoa mchango wao katika kupunguza matatizo yanayowakabili.
 
Alisema wanawake ndio wazalishaji mali katika ngazi ya familia na taifa, kwani wao ndio walezi, lakini kutokana na mila na utamaduni huko nyuma, wanawake walikosa fursa za kumiliki mali, kupata elimu na za uongozi na hivyo kujikuta wakiachwa nyuma kimaendeleo.
 
Alisema asilimia 80 ya wanawake nchini wanaishi maisha duni, hasa walioko vijijini ambako wanategemea kilimo cha jembe la mkono na wengi wao hawana elimu ya ujasiriamali wala mitaji kukuza biashara zao.
 
WAMA, alisema, ina malengo sita ambayo yataweza kuwasaidia wanawake katika kuleta maendeleo. Aliyataja kuwa ni pamoja na kutafuta fursa za elimu ya mtoto wa kike katika ngazi zote, kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa wanawake wajawazito na vifo vya watoto.
 
Malengo mengine ni kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi, kutetea usawa wa kijinsia katika ngazi zote za jamii, kutafuta fursa za elimu na rasilmali zitakazomkomboa mwanamke kifikra na kiuchumi na kutetea mila ma desturi nzuri na kupiga vita zilizopitwa na wakati zinazohatarisha maisha ya mwanamke.
 
Mama Salma alisema hapana budi kupambana na baadhi ya mila na desturi zinazochangia kueneza maambukizi ya virusi vya ukimwi. Takwimu, alisema, zinaonyesha kwamba asilimia 7.7 ya wanawake wanaishi na virusi, huku wanaume wakiwa ni asilimia 6.3.
 
Aliwataja wajumbe wa bodi ya WAMA kuwa ni mke wa Makamu wa Rais, Mama Mwanamwema Sheni, mke wa Waziri Mkuu, Regina Lowassa, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, aliyekuwa Mbunge wa Afrika Mashariki, Hulda Kibacha, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mwanaidi Sinare na Mhasibu Mkuu wa Serikali, Blandina Nyoni.
 
Katika uzinduzi huo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, ambaye alisema serikali zote mbili zimekuwa mstari wa mbele katika kupigania maendeleo ya wanawake kwa kuhakikisha wanapata haki na fursa sawa za elimu.
 
Alisema serikali kwa kumtambua mtoto wa kike hapati fursa ya elimu sawa na mtoto wa kiume, zilianzisha mpango wa kuwasaidia elimu ya sekondari watoto wa kike, hasa wanaotoka familia maskini.
 
Rais Karume alisema mpango huo umeleta mafanikio makubwa Tanzania Bara kwani jumla ya watoto 4,750 kutoka familia maskini na yatima walijiunga na elimu ya sekondari kati ya mwaka 1996 na 2001.
 
Alisema watoto 409 walijiunga na elimu ya juu ya sekondari, 50 walijiunga na vyuo vya ufundi na 266 walichaguliwa kwenda vyuo vya ualimu na wachache walijiunga na vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu. Rais Karume pia alizindua tovuti ya WAMA.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by ngemera)
    Rating
    This is a dirty way of swindling our money. Why today when the hussy becomes a president? Indeed this is but a hoax.
    Stop this nonsense.
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.