Ataka maeneo yaliyobomolewa vibanda yapandwe miti na maua
Kampeni ya kuliweka jiji safi iendelee kwa kasi mpya
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Edward Lowassa amewaagiza viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam, jiji na manispaa kuhakikisha kuwa wachuuzi wa biashara ndogo ndogo (machinga) hawarudi tena kwenye maeneo walikoondolewa hivi karibuni.
Ameagiza pia kuwa maeneo yaliyobomolewa vibanda vya biashara yasafishwe na kupandwa miti au maua kuboresha mandhari na yasiwe kivutio tena kwa waliohamishwa kurudi, na kwamba kampeni ya kuliweka jiji safi iendelee “kwa kasi kubwa zaidi”.
Lowassa ametoa maagizo hayo katika barua yake ya juzi kwa viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam, jiji na manispaa tatu za Ilala, Kionondoni na Temeke kuwapongeza kwa kufanikisha operesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara hao katika maeneo wasikoruhusiwa na kupangiwa maeneo maalum.
Alisema wananchi wengi wa Dar es Salaam sasa wanaona manufaa ya kutekelezwa kwa operesheni hiyo kwa kuwa barabara sasa ni wazi zaidi, na hivyo kupungumza msongamano, na vile vile kazi ya kuweka Jiji katika hali ya usafi sasa ni rahisi zaidi.
“Kukiwepo na uongozi wa pamoja, umakini na wananchi wakielimishwa kutambua faida za hatua mbalimbali za serikali, hakuna ulazima wa kutumia nguvu katika kutekeleza majukumu, hata yale magumu kama hilo la kuwaondoa wananchi wanaokiuka sheria na kanuni za uendeshaji miji,” alisema.
“Uongozi wa mkoa umefanya kazi hii kwa pamoja na kama timu moja. Mmewaelimisha wananchi na mmewaondoa kwa ustaarabu mkubwa sana. Wapo waliokuwa wanahofu kutokea fujo katika utekelezaji wa kazi ya kuwaondoa wafanyabashara ndogondogo,” aliongeza.
Lakini, Waziri Mkuu Lowassa aliwaonya viongozi hao “kuhakikisha kuwa wafanyabiashara hawarudi tena kwenye maeneo hayo na mengine ambayo hayakutengwa kwa matumizi ya biashara ndogondogo.
Kampeni ya kuweka jiji katika hali ya usafi iendelee kwa kasi kubwa zaidi…Nawapongeza tena na kuwataka muendelee kwa ari na kasi hiyo mliyoionyesha”.
Maelfu ya wafanyao biashara ndogondogo mapema mwezi huu waliondolewa katika sehemu ambazo hazikupangwa kwa biashara hiyo na kupelekwa kwenye maeneo maalum yaliyopangwa, katika operesheni iliyofanikiwa ambayo halijapata kutokea katika historia ya jiji la Dar es Salaam.
Machi, mwaka huu, Waziri Mkuu alitoa miezi sita hadi Septemba 30 kwa viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam , jiji na manispaa tatu kuhakikisha kuwa wanawaondoa wafanyabiashara hao waliokuwa wamezagaa ovyo na kuwahamishia kwenye maeneo maalum yaliyotengwa.
Hatua hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya kuondoa msongamano katika Jiji na kuweka mandhari yake yawe safi .
Vibanda mbalimbali vya biashara vilivyojengwa ovyo katika maeneo yasiyostahili vilibomolewa baada ya baadhi ya wenyewe kushindwa kutimiza ahadi ya kuvibomoa ilipofika Septemba 30.
Kumekuwepo na “bomoabomoa” ya vibanda vya machinga na wafanyabiashara wengine wadogo wadogo huko nyuma, lakini operesheni ya sasa inaonekana imefanikiwa zaidi kuliko za awali.