.Ni baada ya kumtapeli mfanyabiashara kiasi cha shilingi milioni moja
.Yavalia mavazi ya kipadre kufanikisha wizi wao
.Mapadre wasikitishwa naeneo la kanisa kuhusishwa na vitendo vya utapeli
Majambazi wawili wanaodhaniwa kuwa na mtandao wa kitaifa wamekamatwa mjini Kibondo baada ya kumtapeli mfanyabiashara mmoja kiasi cha shiulingi milioni moja na kutokomea nazo kabla ya kutiwa mbaroni.
Waliokamatwa ni Bw. Michael Eleneo Langinya (45) Mhehe mkazi wa mkoa wa Ishindo mkoa wa Iringa pamoja na John Athanas (30) mfipa mkazi wa mkoa wa Mbeya ambao waliingia wilayani Kibondo octoba 23.
Wakihojiwa na jeshi la polisi watuhumiwa hao wamekiri kuingia wilayani Kibondo wakitokea wilaya ya Kasulu ambapo wamedai kuwa walikuja kuleta taarifa za msiba wakitokea mkoani mbeya.
Taarifa za uchunguzi wa polisi zinasema kuwa, majambazi hayo yasiyotumia silaha ambayo yanadaiwa kupora mamilioni ya fedha sehemu mbalimbali nchini, yalifika kwa mfanyabiashara Mstafa Nsumyi na kunadi biashara ya magendo ya saruji na mabati.
Imedaiwa kuwa wakiwa nyumbani kwa Bw. Nsumyi waliongea na mmoja wa mafundi Bw. Ansa Nkoko na kumtaka amwambie tajiri yake kuwa wao wanauza saruji na mabati kwa bei ya magendo a kumwachia mawasiliano ya simu.
Imebainishwa kuwa baada ya Bw. Nsumyi kurejea nyumbani alihabarishwa juu ya habari hiyo na kasha kuwapigia simu matapeli hao ambao walidai kuwa watumishi wa kanisa katoliki parokia ya Kibondo.
Aidha Bw. Mstafa Nsumyi aliwafuata majambazi hao eneo la kanisa katoliki ambapo alikutana nao na mmoja wao alikuwa amevaa mavazi ya kichungaji kuashiria kuwa yeye ni padre wa kanisa hilo.
Katika harakati za uporaji huo, Bw. Michael Langinya ambaye aliva mavazi ya kichungaji alimtaka Bw. Nsumyi anunue saruji na Mabati ambayo alidai kuwa yamesalia katika ujenzi wa shule ya awali ya kimataifa ya Kumgarika inayojengwa na kanisa katoliki wilayani Kibondo.
Bw. Nsumyi bila hata kuhoji aliwakabidhi kiasi cha shilingi moja na kasha kukaa maeneo ya kanisani kusubiri mzigo wake lakini hali ilikuwa tofauti alipokwenda kuuliza kwa mapadre na kuambiwa kuwa hawatambua suala hilo.
Bw. Nsumyi alitoa taarifa kituo cha polisi ambapo kwa ushirikiano na raia wema watuhumiwa hao walikamatwa katika kituo cha mapasi cha Kakonko wekielekea Nyakanazi.
Wakihojiwa na jeshi la polisi matapeli hao wamekiri kupokea kiasi hicho cha pesa kutoka kwa Bw. Mstafa Nsumyi na kukiri kuwa walikuwa na nia ya kumuuzia saruji na mabati ya wizi, ingawa wamemtuhumu Bw. Mstafa kuwa hakupaswa kutoa pesa hizo kwani anajua maduka ya vifaa vya ujenzi yalipo.
Aidha mapadre wa kanisa katoliki parokia ya Kibondo wamesikitishwa na kitendo cha matapeli kutumia mavazi ya kichungaji na maeneo ya kanisa lao kuendesha shughuli za kuwatapeli wafanyabiashara.
Wamekiri kuwepo kwa matukio kadhaa katika maeneo ya kanisa lao na wameonya wafanyabiashara kukubali kienyeji kutapeliwa na watu wasio wajua na kutotoa taarifa kwa uongozi wa kanisa hilo.
Hii ni mara ya tano kwa watu waliojulikana kuwatapeli wafanyabiashara wilayani Kibondo kwa madai ya kuwauzia vitu vya magendo ambapo wafanyabiashara hao(majina yao yanahifadhiwa) wamekuwa na desturi ya kukubali kuuziwa bidhaa zisizo na stakabadhi na za wizi.
Watuhumiwa hao ambao polisi inatarajia kutangaza habari zao nchi nzima wanatarajiwa kufikishwa mhakamani wiki hii baada ya uchunguzi juu ya tuhuma zao kukamilika