POLISI inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za utapeli, mmoja akitenda kosa hilo akiwa amevalia kama padre.
Watuhumiwa hao walikamatwa mjini Kibondo, baada ya kumtapeli sh. milioni moja mfanyabiashara Mustafa Nsumyi.
Waliokamatwa ni Michael Langinya (45), mkazi wa Ishindo mkoani Iringa na John Athanas (30), mkazi wa mkoa wa Mbeya, ambao waliingia wilayani Kibondo, Oktoba 23, mwaka huu.
Wakihojiwa na Jeshi la Polisi watuhumiwa walikiri kuingia wilayani Kibondo wakitokea wilaya ya Kasulu, wakidai kuwa walitoka Mbeya kwa ajili ya kuwasilisha taarifa ya msiba.
Ilidaiwa kuwa wakiwa nyumbani kwa Nsumyi, walizungumza na mmoja wa mafundi wake, Ansa Nkoko, wakimtaka amwambie tajiri yake kuwa wao wanauza saruji na mabati kwa bei ya magendo na kumwachia namba zao za simu.
Baada ya Nsumyi kurejea nyumbani, alielezwa habari hiyo na aliwapigia simu matapeli hao, ambao walidai kuwa watumishi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kibondo.
Nsumyi aliwafuata matapeli eneo la kanisa na kukutana nao, mmoja akiwa amevaa kama padre kuashiria kuwa yeye ni padre wa kanisa hilo .
Katika harakati za utapeli huo, Langinya ambaye alivaa mavazi ya padre, alimtaka Nsumyi anunue saruji na mabati aliyodai yamebakia katika ujenzi wa shule ya awali ya kimataifa ya Kumgarika, inayojengwa na Kanisa Katoliki wilayani Kibondo.
Inadaiwa Nsumyi bila kuhoji aliwakabidhi sh. milioni moja na aliendelea kukaa maeneo ya kanisani akisubiri mzigo wake, lakini hali ilikuwa tofauti alipokwenda kuuliza kwa mapadre na kuambiwa kuwa hawatambui suala hilo .
Nsumyi alitoa taarifa kituo cha polisi, ambapo kwa ushirikiano na raia wema watuhumiwa hao walikamatwa katika kituo cha mabasi cha Kakonko, wekielekea Nyakanazi.
Walipohojiwa polisi, matapeli hao walikiri kupokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Nsumyi na kwamba walikuwa na nia ya kumuuzia saruji na mabati ya wizi
Mapadre wa kanisa hilo wameeleza kusikitishwa na kitendo cha matapeli kutumia mavazi ya kichungaji na maeneo ya kanisa kuendesha shughuli za kuwatapeli wafanyabiashara.