Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, amelitaka Baraza la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), kuwa na programu za kuendeleza vipaji chipukizi ili kuinua kiwango cha mchezo huo.
Rais Kikwete alisema hayo jana, muda mfupi kabla ya kuanza kwa mchezo wa fainali ya Kombe la Kagame, kuwania ubingwa wa klabu za nchi za ukanda huo, kati ya wenyeji Moro United na Polisi Uganda, Uwanja wa Taifa, jijini.
’Msiishie tu kuandaa mashindano, lazima muwe na programu za kuendeleza mchezo huu, na hasa kuanzia kule kwa chipukizi wetu,’ alisema Kikwete.
Katika hilo, Rais huyo wa serikali ya Awamu ya Nne, alisema serikali yake iko tayari kutoa kikombe cha mashindano ya watoto wa nchi za mataifa hayo, akitoa changamoto kwa CECAFA kutafuta wadhamini wengine ili kuyaanzisha.
Kauli ya Kikwete inatokana na ukweli kuwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, zimekuwa nyuma katika maendeleo ya mchezo huo, hali ambayo ni tofauti na kanda nyingine za Afrika.
Kanda za Afrika Magharibi, Kaskazini na Kusini zimekuwa na kiwango kizuri na mara nyingi ndizo zinazotawala Bara la Afrika za fainali za Kombe la Dunia.