Na Peter Orwa
SERIKALI kuanzia Desemba mwaka huu, itaanza kugawa viwanja 5,000 vinavyoendelea kupimwa katika eneo la Kibada, wilayani Temeke.
Meneja wa Mradi wa Upimaji Viwanja 20,000 jijini Dar es Salaam, Venant Mugemuzi, aliliambia gazeti hili jana kuwa, hadi sasa vimeshapimwa viwanja 2,861 na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika kabla ya Desemba.
Alisema upimaji viwanja vya Kibada, unafanywa na tatasisi tatu, mbili za serikali na moja binafsi ambazo hakuzitaja.
Kwa mujibu wa Mugemuzi, gharama za kulipia kiwanja itatokana na gharama iliyotumika katika kazi ya kupima, kwani ndio mtindo unaotumika katika kutoza gharama za kulipia kiwanja.
Wiki hii, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ilitangaza ugawaji wa viwanja 281 eneo la Kinyerezi.
Hata hivyo, taarifa kutoka wizara hiyo, ilisema viwanja vya Kinyerezi vimegawiwa chini ya uratibu wa mradi wa viwanja 20, 000, ingawa havimo katika mradi wenyewe.
Mugemuzi alisema serikali inaendelea kugawa viwanja katika eneo la Buyuni, wilayani Ilala ambapo hado vimebakia wastani wa viwanja 2,000 kati ya 5,000 vilivyopo.
Alisema baadhi ya wafanyakazi wa serikali waliojiunga kupitia wizara zao kwa pamoja wamekuwa wakifika kuchukua fomu.
Mugemuzi alitoa mfano wa Wizara ya Mambo ya Ndani wamechukua fomu za viwanja 1,807 na Mfuko wa Akiba ya Mashirika ya Umma, imechukua fomu 500.
“Katika mwaka huu wa fedha, Kibada ndiyo eneo la mwisho,” alisema Mugemuzi na kuongeza kuwa baada ya hapo serikali itaelekeza nguvu zake katika mikoa ya Morogoro na Mwanza.