Na Furaha Omary
NCHI wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) zimepewa changamoto ya kushirikiana kukabiliana na umasikini uliokithiri, ujinga na maradhi.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Asha Rose Migiro wakati wa maadhimisho ya miaka 61 ya UN, yaliyofanyika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
Dk. Asha Rose alisema: “Umasikini uliokithiri ndio changamoto inayokwamisha juhudi za Umoja wa Mataifa kufikia malengo yake ya Milenia ya 2015.”
Alisema kwa sasa duniani watu zaidi ya bilioni 1.3 wanaishi kwa matumizi ya chini ya dola moja kwa siku.
Mratibu Mkazi wa UN, Oscar Fernandez, alitaka maadhimisho hayo yatumike kutathmini mafanikio na pia kupanga malengo ya kimaendeleo.
Fernandez aliisifu Tanzania kutokana na uwezo walionao viongozi wake kiutendaji, hali inayoendelea kuiweka kuwa nchi ya amani na utulivu.