Na Epson Luhwago
RAIA wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Nura Mwemedi Babou (37) na Mtanzania, Abubakar Khalid (47), jana walifikishwa katika mahakama ya wilaya ya Ilala,
Dar es Salaam, kwa tuhuma za kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuishi nchini kinyume cha taratibu.
Mwendesha mashitaka, Mrakibu wa Polisi Germanus Mhume, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mustafa Mlawa kuwa Babou, Khalid na wenzao ambao hawajakamatwa, Septemba 21, mwaka jana mjini Dar es Salaam, kwa pamoja walikula njama za kujipatia fedha kwa udanganyifu.
Katika shitaka la pili, Mhume alidai kuwa kati ya Septemba, mwaka jana na Agosti 31, mwaka huu, washitakiwa wakiwa katika ofisi za Efficient Freighters (T) Limited, walijipatia dola 66,446 (sh. 84,254,200) kutoka kwa mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, Siril Makoy.
Mhume alidai kuwa washitakiwa waliomba fedha hizo kutoka kwa Makoy na kupewa kama mkopo kwa makubaliano kuwa wangezirejesha baada ya kuuza madini aina ya ‘tantalite’ yaliyokuwa katika makontena yaliyokuwa yakisubiri kusafirishwa kwenda nje wakati wakijua
kuwa hayakuwa madini bali mchanga tu.
Katika shitaka lingine, ilidaiwa kuwa tangu mwaka jana, Babou amekuwa akiishi nchini kinyume cha sheria za uhamiaji nchini kwa kuwa hati zake hazionyeshi kama aliingia kwa kufuata taratibu na sheria za nchi.
Vile vile raia huyo wa DRC amedaiwa kuishi nchini bila kibali, hivyo kukiuka taratibu na sheria za uhamiaji, hali ambayo ilisababisha kukamatwa na polisi.
Washitakiwa walikana mashitaka yote na wako nje kwa
dhamana hadi Novemba 11, mwaka huu, kesi itakapotajwa.
Wameachiwa kwa masharti kwamba kila mmoja atie saini hati ya dhamana ya sh. milioni 20 na kuwa na wadhamini wawili wenye kueleweka kwa dhamana ya thamani hiyo hiyo.
Washitakiwa pia wametakiwa kusalimisha mahakamani pasipoti, hati na nyaraka zote za kusafiria na ukazi. Pia wametakiwa kutotoka nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama.
Pamoja na kupata dhamana hiyo, hali haikuwa rahisi kwani upande wa mashitaka ulisimama kidete kuishawishi mahakama kuwanyima dhamana.
Mhume katika hoja zake alidai kuwa mshitakiwa wa kwanza si raia wa Tanzania, hivyo kupewa dhamana anaweza kukimbia nchini kama ilivyotokea kwa Wacongo wengine ambao wamekuwa wakishitakiwa kwa makosa mbalimbali.
Upande wa mashitaka katika kuomba washitakiwa kutokupewa dhamana ulidai kuwa kuwepo kwao nje ya dhamana kunaweza kuvuruga upepelezi wa esi ambao haujakamilika.
Hata hivyo, wakili wa utetezi, Jerome Msemwa, alidai washitakiwa wana haki ya kupata dhamana kwa kuwa wa kwanza amekuwa mikononi mwa polisi kwa zaidi ya wiki moja na kwamba pasipoti yake imeshikiliwa na polisi, hivyo si rahisi kutoroka.
Kwa upande wa mshitakiwa wa pili, alidai ni mgonjwa na anahudhuria matibabu Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, na sasa amepewa mapumziko ya wiki mbili.
Babou na Khalid walikamatwa na polisi wiki iliyopita kwa njama za kutaka kusafirisha nje ya nchi makontena mawili ya mchanga kutoka Congo waliodai ulikuwa na madini ya tantalite.
Madini hayo yaliyodaiwa kuwemo humo, mali ya kampuni ya Tanganyika Minerals Ltd ya Bukavu, DRC, yalikuwa yauzwe kwa kampuni ya H.H. Metals ya Marekani ambayo baadaye ilighaili na kuamua kuiuzia kampuni ya Impulse International (T) Limited yenye makao makuu India.
Inadaiwa wakati mazungumzo yakiendelea nao walighaili na kuamua kuiuzia kampuni ya Afrika Kusini ambayo ilishindwa kununua baada ya taarifa za maabara ya madini ya kampuni ya Alfred H. Knight (UK) Ltd kuonyesha kuwa hakukuwa na madini yoyote.
Baada ya kampuni ya Afrika Kusini kughaili pia, Khalid kupitia kampuni yake ya Trans Trading Co. Ltd na Tanganyika Minerals walifanya tena mazungumzo na Impulse ambayo ilikubali.
Kabla ya kununua, ilibidi sampuli za mchanga huo zipelekwe Hong Kong kupimwa ili kujua aina ya madini yaliyokuwemo. Taarifa za vipimo zilionyesha hakukuwa na madini yoyote.