HALMASHAURI ya manispaa ya Temeke, Dar es Salaam imesema italifanyia maboresho soko la Tandika ikiwa ni pamoja na banda la samaki wabichi na machinjio ya kuku kabla ya Julai, mwaka huu.
Hatua hiyo inatokana na malalamiko ya wafanyabiashara kudai kuwa wamekuwa wakifanya biashara katika mazingira machafu kutokana na banda la samaki kuchakaa, wakati kuku wanachinjwa chini kwenye mchanga jambo ambalo ni hatari kwa afya.
Uboreshaji wa maeneo ya machinjio ya kuku na banda la samaki wabichi utakuwa umeondoa kero kwa wafanyabiashara hao watakaokuwa wakifanya shughuli zao katika mazingira mazuri sambamba na kuwapatia wateja lishe kutoka katika maeneo yanayozingatia kanuni za afya.
Afisa Uhusiano wa Manispaa ya Temeke, Dar es salaam David Mgonja alimwambia mwandishi wa habari hii katika mahojiano mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba kazi ya kuliboresha soko hilo itafanyika kabla ya Julai, mwaka huu.
Alisema kuwa manispaa inatambua mazingira ya soko hilo kuwa hayaridhishi na kwamba ni kutokana na hali hiyo ndiyo maana wamefikia hatua ya kuliboresha zaidi ili lifikie hadhi ya kuwa soko la kisasa.
Mwandishi wa habari hii alipotembelea soko hilo mwishoni mwa wiki iliyopita aliambiwa na wafanyabiashara hao kuwa manispaa imewatelekeza kwa kuwaacha waendelee kufanya biashara katika mazingira machafu.
Walisema kwamba banda la samaki wabichi limebomoka kutokana na uchakavu na hivyo kuwalazimu kuhamia katika sehemu ya wazi isiyokuwa rasmi yenye mchanga ambayo hujaa tope kutokana na maji ya samaki yanayotiririka wakati wote.
“Hebu litazame banda hili la samaki paa limebomoka, meza zimevunjika, kuku wanachinjwa chini kwenye mchanga hivi kweli inawezekana kufanya kazi katika mazingira ya aina hii, hata Rais Jakaya Kikwete alipofanya ziara ya kushtukiza mwaka huu hawakumpitisha hapa hii ni aibu,” walisema.
Mfanyabishara Selemani Katundu alisema kwamba maeneo ya samaki na kuku hulifanya soko lionekane chafu wakati wote kwa sababu maeneo hayo hayasafishiki kwa kupigwa deki, hasa wakati wa mvua jambo linaloweza kusababisha kufungwa kwa soko wakati makosa ni ya manispaa.
Alisema kwamba mara nyingi manispaa imekuwa ikiahidi kuliboresha soko hilo hasa maeneo ya samaki na machinjio ya kuku ambayo yanatia aibu na kufedhehesha, lakini kadri siku zinavyokwenda hawaoni juhudi yoyote inayofanywa.
Kutoka gazeti la Uhuru
ISSN 0876-3896 NA.19321
Na Mbazigwa Hassan