Kuhusu maandamano
Na Mwandishi Wetu, Kgoma
MADIWANI wa Halmashauri ya manispaa ya Kigoma/Ujiji wameombwa kuvuta subiri kufanya maandamano kwenda kwa muu wa mkoa hadi kesi itakapomalizika.
Kesi iliyopo mahakamani ilifunguliwa na wafanya biashara ya chumvi toka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kwa ajili ya kuzuia utozwaji wa ushuru wa chumvi wanayosafirisha kwenda nchi hizo mpaka itakapotolewa hukumu.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kanali Joseph Simbakalia kupitia kwa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma John Mongela kwa kuwataka madiwani kutofanya maandamano ya kwenda kumuona mkuu huyo wa mkoa hadi kukamilika kwa maamuzi ya mahakama
Simbakalia alisema hana nia mbaya ya kuwazuia madiwani kufanya maandamano kwa kuwa wapo kwa ajili ya kuwatetea wananchi na wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji lakini lazima kuheshimu maamuzi ya mahakama
Alifafanua kuwa madiwani hao ni wa kwake na kamwe hatathubutu kuwatenga kwa kuwa ni watu muhimu wa kufanya nao kazi katika suala zima la kuwaletea maendeleo wananchi lakini ni muhimu kuiheshimu mahakama katika maamuzi yake.
Hata hivyo, mkuu wa mkoa amewaambia madiwani hao kuwa baada ya hukumu hiyo kutolewa itakuwa ni muda muafaka wa kukaa nao kwa ajili ya kulizungumzia suala hilo kwa kina.
Kesi hiyo ya kuzuia utozwaji wa ushuru wa chumvi ambayo ipo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma ilifunguliwa na Husseni Beji kwa niaba ya wafanyabiashara hao wa nchi jirani na inategemewa kutolewa hukumu Novemba 7 mwaka huu baada ya kesi hiyo kudumu kwa miezi saba sasa
Kwa upande wao, madiwani hao walisema hawana budi kukubaliana na mkuu wa mkoa kutokana na ushauri alioutoa kwani anaonyesha ni jinsi gani alivyokuwa na moyo wa kuwasaidia wakazi wa Mkoa wa Kigoma