Na Deo Nsokolo, Kigoma
MCHUNGAJI wa kanisa ametiwa mbaroni akitaka kuitapeli mamilioni ya shilingi Manispaa ya Kigoma/Ujiji.
Samson Ntimbo, mchungaji wa United African Fellowship Church, mjini Kigoma, alitiwa mbaroni Jumamosi iliyopita muda mfupi kabla ya manispaa ya Kigoma/Ujiji na mchungaji huyo kutia saini mkataba unaodaiwa kwamba ulikuwa bandia, wa ujenzi wa zahanati ya Kikunku, kata ya Gungu, na kukifanya kituo cha afya.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kigoma, Patrick Byatao, amesema polisi inaendelea na uchunguzi kabla ya kumfikisha mahakamani kwa kosa la kutaka kujipatia pesa kwa udanganyifu.
Alidai kwamba kati ya Mei na Oktoba 20 mwaka huu mtu huyo amekuwa akitiliana saini na idara ya afya ya manispaa mikataba na uongozi wa manispaa ya kuanzisha kamati ya maendeleo ya kata ya Gungu.
Taarifa zaidi zimedai mchungaji huyo, akiwa na vielelezo vya kughushi kutoka kwa wazungu mbalimbali aliodai kuwa ni wachungaji wa kanisa hilo nchini Australia, alieleza kuwa shirika lake limeanzisha mradi wa kuiboresha zahanati ya Kikunku ili iwe kituo cha afya na chuo cha afya, jambo ambalo lilipokewa na manispaa.
Chini ya mradi huo, sh. milioni 200 zilitarajiwa kutumika ambapo Manispaa ilitakiwa kutoa sh. milioni 20 ukiwa mchango wake. Katika uboreshaji wa zahanati hiyo, vyumba vinane vilikusudiwa kujengwa.
Vyumba hivyo ni pamoja na wodi mbili mbili kwa ajili ya akina mama, wanaume, watoto na vyumba viwili, kimoja cha daktari na kingine darasa kwa wauguzi.
Inadaiwa nia ya kiongozi huyo ilikuwa ni kupata kiasi hicho cha sh milioni 20 kutoka manispaa baada ya kuonyesha vielelezo vyake na kuelekeza uwekaji wa fedha hizo benki.
Hata hivyo, katika hatua za mwisho za kukamilisha mkataba ili utiwe saini kuhusu mradi huo baina ya Ntimbo na uongozi wa juu wa manispaa, chini ya mkurugenzi wa manispaa, Shabani Ntalambe na mganga wa manispaa Shaaban Mkoko, ulijitokeza wasiwasi baada ya kubainika kuwa tangu kuanza kwa mchakato wa mkataba huo ni mtu huyo pekee aliyeonekana kulizungumzia suala hilo bila ya kuwaonesha watendaji wengine.
Baada ya kumhoji, Ntimbo aliwachukua baadhi ya viongozi hao hadi katika eneo la NORAD mjini hapa ambako alidai ndiko waliko wakuu wake wa kazi hizo. Walipofika katika eneo hilo, inadaiwa mchungaji huyo alidai bosi wake, ambaye pia ni mchungaji wa madhehebu yake, alikuwa ameondoka kwa ndege kurudi kwao Australia kwa mipango zaidi ya mradi.
Baada ya kuona hali hiyo ujumbe wa watu hao uliwahoji baadhi ya watu wa eneo hilo ambao walisema hawamjui wala kuwepo kwa viongozi na kanisa la watu hao.