WAKUU wa nchi za Jumuiya ya Uchumi ya Kusini mwa Afrika (SADC), wameipitisha kwa kauli moja ripoti ya hali ya kisiasa na usalama ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) iliyotayarishwa na chombo ambacho mwenyekiti wake ni Tanzania.
Ripoti hiyo iliwasilishwa na kusomwa kwenye mkutano mkuu maalumu wa SADC wa siku moja mjini hapa juzi na Waziri Mkuu Edward Lowassa, akimwakilisha Rais Jakaya Kikwete.
Kamati ya mawaziri iliyoandaa ripoti hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Dk. Asha-Rose Migiro, ni ya chombo cha ushirikiano katika masuala ya siasa, ulinzi na usalama cha SADC.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa tathmini iliyofanywa ya hali ya kisiasa, kiulinzi na kiusalama, kwenye demokrasia hiyo ni shwari kwa ajili ya kufanyika kwa uchaguzi wa rais kwa raundi ya pili wiki ijayo.
Ilieleza kuwa kukamilika kwa shughuli ya Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo hakutamaliza machafuko ila jitihada zaidi zinatakiwa kuimarisha utulivu na amani ya nchi hiyo.
Mara baada ya Waziri Mkuu Lowassa kusoma ripoti hiyo , wakuu wa nchi waliipokea kwa kauli moja na kuipongeza Tanzania kwa kukiongoza vizuri chombo hicho cha SADC cha ushirikiano katika siasa, ulinzi na usalama.
Wakuu wa nchi hizo walikubaliana kuharakisha mpango wa kuziunganisha kiuchumi nchi za SADC, ili kuendesha biashara kwenye nchi hizo kwa uhuru zaidi ifikapo mwaka 2008 na kuwa na Umoja wa Forodha ifikapo mwaka 2010.
Kabla ya mkutano huo kufungwa, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Rais Festus Mogae wa Botswana na Waziri Mkuu, Absalom Dlamini wa Swaziland walitia saini mkataba wa kujiunga na Kamati ya Fedha ya SADC.