VYAMA vya hiari nchini Zimbabwe, vimemkataa Rais mstaafu Benjamin Mkapa, kuwa msuluhishi wa mgogoro wa kisiasa nchini humo, ambao umesababisha uvunjifu wa haki za binadamu kwa kiwango kikubwa.
Mratibu wa muungano wa vyama hivyo vya hiari nchini Zimbabwe, Mchungaji Nicholas Mukaronda, aliiambia Tanzania Daima jana katika ofisi za Kituo cha Haki za Binadamu nchini, kwamba Zimbabwe ina mgogoro mkubwa wa kisiasa unaohitaji usuluhishi, lakini hawapo tayari kusuluhishwa na Mkapa, kwa madai kuwa tayari msimamo wake kwa Rais Robert Mugabe unajulikana.
Mchungaji huyo yupo nchini, akiongoza ujumbe wa viongozi wengine wanne ambao watakuwa na semina ya siku mbili na vyama vingine vya hiari nchini, kujadili na kubadilishana mawazo jinsi ya kukabiliana na tatizo la uvunjifu wa haki za binadamu nchini Zimbabwe.
Wajumbe wengine walioambatana na Mukaronda ni Jestina Mukoko, Elinor Sisulu na Jacob Mafume.
Alisema tayari muungano wa vyama hivyo unaojumuisha vyama 350, walishamwona Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe kumwelezea azima ya kutomkubali Rais mstaafu Mkapa kuwa msuluhishi wa mgogoro huo.
“Tunasikia Mkapa ameteuliwa na Rais Mugabe kuwa msuluhishi wa mgogoro wa kisiasa nchini Zimbabwe. Sisi tunasema hatumtaki, na tumeshaonana na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, naye amesema baada ya uteuzi rasmi, vyama hivyo vinaweza kukutana na Mkapa kwa majadiliano kabla ya kuanza usuluhishi,” alisema Mchungaji Mukaronda.
Alisema mara baada ya kusikia kwamba Mkapa atakuwa msuluhishi wa mgogoro huo, vyama hivyo vimefanya uchunguzi na kumpeleleza Rais Mkapa kuanzia sehemu alikozaliwa ili kujua undani wake na wamebaini kuwa Mkapa anaweza kumlinda Rais Mugabe, aliyemwelezea kuwa swahiba wake.
Hata hivyo, alisema vyama hivyo kwa sasa vinasubiri uteuzi rasmi wa Mkapa kuwa msuluhishi ili viweze kutoa mapendekezo juu ya usuluhishi wake katika mgogoro huo.
Mchungaji huyo alikumbushia jinsi Rais Mkapa alivyokuwa wa kwanza kutoa taarifa ya kumpongeza Mugabe kwa ushindi wake, kwamba uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, wakati nchi nyingi, zikiwamo za Afrika zilisita kutoa kauli yoyote ya kuunga mkono ushindi huo.
Alisema vyama hivyo vya hiari vitaridhika endapo msuluhishi wa mgogoro huo atakuwa Rais mstaafu wa Msumbiji, Joaquim Chisano, ambaye aliteuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) kusuluhisha mgogoro huo, lakini Rais Mugabe akamkataa.
Kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Zimbabwe, Mafume ambaye ni mratibu wa vyama hivyo vya hiari, alisema kuwa hali ni mbaya, kwani hivi sasa kila kitu kinakwenda kijeshi na polisi wote wanafanya kazi kwa maagizo ya chama tawala.
“Ukitaka kuwa rafiki wa serikali, uwe mwanachama wa chama tawala, kama uko upinzani, unachukuliwa kuwa ni mhalifu,” alisema.
Aliongeza kuwa, wanafunzi ambao wazazi wao ni wanachama wa vyama vya upinzani, wanashindwa kusoma na wakati mwingine wanafanya mitihani yao ya mwisho wakiwa polisi kwa sababu alizodai kuwa ni za uonevu.
Rais mstaafu Mkapa amepata kumpongeza Rais Mugabe na kumtetea kwenye majukwaa ya kimataifa, kwa sera yake tata ya kuwapokonya Wazungu ardhi na kuwapa Waafrika.