Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kikwete aomba radhi umeme kukosekana
Kikwete aomba radhi umeme kukosekana
By Habari Tanzania | Published  10/25/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Lucy Ngowi

RAIS Jakaya Kikwete amewaomba radhi Waislamu na Watanzania kwa ujumla kutokana na usumbufu mkubwa walioupata kutokana na kuongezeka kwa makali ya tatizo la umeme katika miezi ya hivi karibuni.

Kikwete aliomba radhi hiyo ya kwanza ya aina yake kwa kiongozi mkuu wa nchi, jana wakati akilihutubia Baraza la Idd el Fitr, lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na kufanyika kitaifa jijini Arusha.

Alisema yeye na wenzake serikalini wanafahamu vyema kwamba, ukosefu wa umeme uliwakarahisha Waislamu wengi hasa pale ulipokosekana wakati wa sala au wakati wa kuandaa futari au daku.

“Tatizo la ukosefu wa umeme hapa nchini ni tatizo linalotusikitisha na wakati mwingine linalotusononesha sana. Tunaomba radhi kwa usumbufu mlioupata kama vile ambavyo tunawataka radhi Watanzania wengine wote kwa usumbufu wanaoupata kutokana na tatizo hili la umeme.

“Ni tatizo la Watanzania wote na wala halikubagua misikiti au Waislamu pekee. Napenda kuwahakikishia kwamba kiini cha tatizo si uzembe wa mtu yeyote bali ni mitihani ya Mwenyezi Mungu kutokutupatia mvua za kutosha na hivyo kusababisha mabwawa yetu ya kuzalisha umeme ya Mtera na Kidatu kutopata maji ya kutosha kuzalisha umeme wakati wote wa mwaka,” alisema.

Rais alisema ni bahati mbaya kwamba tatizo hilo la umeme halina majawabu ya papo kwa papo, tofauti na yalivyo matatizo mengine kama njaa, ambayo yanaweza kutatuliwa na kuwapo kwa fedha za kuagiza chakula.

Hata kwa umeme wa dharura imechukua miezi isiyopungua mitano tangu uanze mchakato wa kukodi mitambo ya kuzalisha umeme.

“Ni sasa tu ndipo baadhi ya mitambo imewasili na baadhi imeanza kazi. Ni matumaini yetu kwamba ifikapo mwishoni mwa mwezi ujao au hata katikati karibu mitambo yote ya kukodi itakuwa imewasili na kuanza kuzalisha umeme,” alisema Rais Kikwete.

Pamoja na kuwasili kwa mitambo hiyo mwezi ujao, Kikwete alisema jawabu hasa la tatizo hili litakuwa limepatikana mwakani wakati mitambo mipya ya Tanesco ya Ubungo na Tegeta itakapokuwa imeanza kutoa umeme.

Rais aliwasihi Watanzania kuendelea kuwa wavumilivu na wenye moyo wa subira wakati serikali inaendelea kukabiliana na tatizo hili.

“Naelewa hisia ya mtu mwenye tatizo kubwa anayesubiri jawabu la haraka kila unapomwambia awe na subira anaona humpatilizi,” alisema.

Aliwahakikishia Watanzania kwamba, serikali yake imekuwa ikilifuatilia kwa karibu tatizo hilo na wakati mwingine wamekuwa wakilazimika kukesha wakihangaikia suala hilo hilo.

Alisema kwa ujumla anaridhika na jitihada zinazofanywa na viongozi na watendaji serikalini na mashirika husika katika kukabiliana na tatizo hili.

Alikiri kuwapo kwa ulegevu na makosa ambayo serikali imekuwa ikiyachukulia hatua kila ilipoyabaini, na amebainisha kuwa serikali haitasita kuchukua hatua zaidi kama hapana budi.

Akizungumzia mahusiano ya kidini, alisema kumekuwapo watu wachache au vikundi vichache vya watu katika jamii wanaopenda kuchochea uhasama na kutoelewana kati ya Waislamu na Wakristo au kati ya taasisi na madhehebu tofauti ya Wakristo na Waislamu.

“Nataka kuwahakikishia kwa mara nyingine tena Watanzania wenzangu kuwa serikali haitawaachia hawa watu wakorofi au waovu wachache waivuruge nchi yetu. Wakati wote tutakuwa macho na makini kuhakikisha kuwa hawapati fursa ya kufanya uovu wao. Tumefanikiwa miaka yote huko nyuma, hatuwezi kushindwa sasa,” alisema.

Katika hotuba hiyo, Kikwete hakusita kulikumbusha Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kuwa siku za nyuma halikuwa na sifa nzuri kwa upande wa usimamizi na udhibiti wa fedha na mali zake.

Alisema uaminifu wa uongozi na watendaji wa baraza umekuwa unatiliwa shaka kiasi cha kuwafanya watu wengi wenye uwezo kuchelea kuchangia masuala ya Waislamu kupitia katika baraza hilo.

Alisema matokeo yake ni kukosekana kwa misaada muhimu kutoka kwa watu wenye nia njema nchini na hata kwingineko duniani.

“Hivyo kuwa na mfumo mzuri wa usimamizi wa fedha na mali za baraza na kuwa na uaminifu katika usimamizi na matumizi ya fedha na mali za baraza ni jambo la msingi,” alisema Kikwete.

Aliliambia baraza hilo kuwa lazima pawepo na kuaminiwa na kuaminika ndipo wafanikiwe.

Alisema akiwa rais anajisikia mtu mwenye bahati kubwa kupata nafasi ya kuliongoza taifa lenye wacha Mungu wengi na waumini wa dini na madhehebu mbalimbali.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.