Lengo la utoaji wa misaada hiyo kwa taasisi mbalimbali hususani zile za kielimu ni kama njia ya shukurani kwa Watanzania ambao ndio wanamiliki asilimia sabini ya hisa za benki ya CRDB.
Mkurugenzi wa shughuli za kibenki za CRDB Tanzania, Bw. Joseph Witts anasema kuwa wakati benki hiyo ikielekea katika kilele cha sherehe rasmi zitakazofanyika mwezi ujao, imeamua kwa kiasi kikubwa kufadhili sekta ya elimu kama ndiyo jibu sahihi la kutatua matatizo mbalimbali ya wananchi kwa njia ya elimu.
’Tumelipa kipaumbele suala la elimu tukiamini kuwa, bila elimu ufumbuzi wa matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii ya Watanzania hauwezi kupatikana. Hata hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alitoa mchango mkubwa wa ukombozi kwa kutupatia elimu’ anasema Bw.Witts na kuongeza kuwa
’Bila elimu Taifa haliwezi kupata viongozi,wafanyakazi na wafanyabiashara bora na ili nchi yetu iweze kusonga mbele katika nyanja mbalimbali hatuwezi kupuuza suala la elimu kwa vile ni moja ya maadui watatu tunaowapiga vita’.
Misaada hiyo anasema, imeelekezwa hasa katika shule za msingi na sekondari sambamba na vyuo vya elimu ya juu, kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho ni miongoni mwa taasisi za elimu zilizonufaika na mpango huo wa CRDB.
Mkurugenzi huyo, anasema kuwa misaada hiyo iliyotolewa au itakayotolewa imegawanywa katika makundi manne. Chuo kikuu cha Dar es salaam kitajengewa kituo cha sanaa na utamaduni kwa gharama ya shilingi milioni 100..
Makundi mengine ni pamoja na uchimbaji wa mashimo na upandaji wa miti katika shule za msingi zilizoteuliwa kupewa misaada hiyo kwa nchi nzima, utoaji wa vifaa vya elimu kama vile vitabu kwa shule teule za msingi na sekondari Tanzania na kutoa elimu ya mazingira.
Katika mkoa wa Mara, benki hiyo imeamua kutoa misaada yake katika shule ya msingi ya Mwisenge, shule ambayo ni ya kihistoria katika Taifa la Tanzania kwa sababu ndipo mahali ambapo muasisi wa Taifa hili,hayati Mwalimu Nyerere alipata elimu yake ya msingi.
Hii inamaanisha kuwa mipango yake ya kulikomboa Taifa hili toka mikononi mwa makucha ya wakoloni, ilianzia katika shule hiyo ya msingi ya Mwisenge iliyopo mjini Musoma ambayo aliitumia kama dira iliyomsaidia kudai uhuru wa Tanzania.
Benki ya CRDB tayari imekabidhi misaada mbalimbali katika shule hiyo kwenye sherehe zilizofanyika Machi 19 mwaka huu, ambapo misaada yenye thamani ya shilingi milioni tano ilikabidhiwa kwa walimu wakuu wa shule hiyo ikimaanisha Mwisenge A na B.
Misaada hiyo ni pamoja na mashimo ya miti na miche 1000 iliyopandwa siku hiyo,fulana 600 zenye nembo ya CRDB, vitabu vya kiada na ziada 320 na hundi yenye thamani ya shilingi laki tano,misaada iliyokabidhiwa mbele ya mkuu wa mkoa wa Mara, Bw. Isidori Shirima.
Mkuu wa mkoa wa Mara, Bw. Shirima anaipongeza benki hiyo kutimiza miaka kumi tangu ianzishwe Julai mosi 1996 chini ya uongozi wa Mkurugenzi mkuu Dk .Charles Kimei ambapo imepata mafaniko makubwa yanayowafurahisha Watanzania wengi.
’Naupongeza uamuzi kama huu wa CRDB wa kusherehekea kutimiza umri wao tangu kuanzishwa kwa kuwashirikisha wananchi na kuwa nao karibu wakati wote. Hii inawapa imani kubwa sana kwamba kweli benki hiyo ni benki ya Watanzania’ anasema.
Anaendelea kusema kuwa kwa kuthibitisha kwamba benki hiyo iko karibu na wananchi wake, hivi karibuni tu imeitikia wito wa Rais Jakaya Kikwete kwa kuungana na makampuni mengine kuchangia fedha za kununua chakula katika mikoa iliyokumbwa na baa la njaa kwa kutoa sh.milioni 20.
Mkuu huyo wa mkoa aliiomba CRDB kuendelea kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa wanaojishughulisha na ununuzi wa mazao ya pamba na kahawa mkoani Mara ambapo mikopo ya benki hiyo isiishie kwa wafanyabiashara tu bali iwafikie na wakulima wa mazao hayo.
’Kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa letu kiuchumi, sasa si jambo la busara wakulima wetu hapa mkoani tukawaacha hivi hivi bila kusikiliza na kutatua matatizo yao hivyo ni matumaini yangu kuwa CRDB itawasikiliza na wao pia’ anasisitiza.
Akizungumzia msaada uliotolewa na benki katika shule ya msingi Mwisenge, Bw. Shirima anasema ni ishara tosha kwamba benki hiyo inajali na kuthamini sana elimu na kuongeza kuwa bila elimu hata benki yenyewe isingeweza kupata wataalam bora ambao wameiletea ufanisi mkubwa.
Anasema tafsiri ya msaada huo ni changamoto kuonyesha kuwa vijana wanatakiwa kusoma kwa bidii zaidi ili baadaye waweze kushika nafasi mbalimbali serikalini ,viwandani,katika kilimo,uvuvi, na wengine katika taasisi za kifedha zikiwemo benki.
Sekta ya elimu mkoani Mara, Bw. Shirima anasema mkoa wake unakabiliwa na matatizo mbalimbali likiwemo suala la upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari jambo ambalo huenda likasababisha kupungua kwa taaluma miongoni mwa wanafunzi katika shule hizo miaka michache ijayo.
Anatoa mfano kwa shule za msingi zipatazo 663 zilizopo mkoani kuwa zina walimu 6731 tu wakati mahitaji halisi ni walimu 8,968 hivyo kuwa na upungufu wa walimu 2237 sawa na uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 63 wakati lengo la kitaifa ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45.
Hivyo anayaomba makampuni mbalimbali hapa nchini ya serikali na yale yasiyo ya kiserikali kuchangia maendeleo ya elimu ili kulikwamua Taifa katika janga la ujinga na hivyo kuwakomboa wananchi kutoka katika giza la umasikini uliokithiri kwa kuwapatia mtaji wa elimu.
Baadhi ya wananchi mjini hapa, wameunga mkono juhudi zinazofanywa na benki ya CRDB hapa nchini za kutoa misaada kwa jamii na kuzitaka benki nyingine ziige mfano huo ambao umefungua njia katika kuleta maendeleo kwa wananchi na Watanzania kwa ujumla kwa vile hiyo ndiyo njia pekee ya kuwashukuru wananchi.
Mkazi mmoja wa mjini Musoma, Bw. Fadhili Janja anasema utaratibu uliotolewa na CRDB unastahili kupongezwa lakini anasema kama benki hiyo inaongozwa na kumilikiwa na Watanzania wenyewe na sasa imepata mafanikio makubwa kumbe haikuwepo haja yoyote ya kubinafsisha benki nyingine za NMB na NBC kwa wawekezaji toka nje ya nchi.
” Hivi serikali yetu ilikuwa na lengo gani la kubinafsisha benki hizo na kuziuza kwa wageni wakati kuna Watanzania wengi wataalam waliobobea katika masuala ya kibenki kama akina Dk Charles Kimei ambao ndiyo walioifikisha CRDB hapa ilipo?”alihoji huku akionekana kusifu kazi nzuri iliyofanywa na mkurugenzi mkuu huyo wa CRDB Tanzania ya kuiboresha benki hiyo.
Benki ya CRDB Tanzania LTD ilianzishwa rasmi Julai Mosi mwaka 1996 baada ya serikali kuamua kuiuza kwa wazawa iliyokuwa Benki ya Ushirika na Maendeleo vijijini(CRDB) hivyo mwaka huu inatimiza miaka kumi tangu ianzishwe.
Yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hicho cha muongo mmoja uliopita moja ya mafanikio hayo yakiwa ni pamoja na kupanda kwa amana ya benki hiyo toka sh. bilioni 40 kwa mwaka 1996 hadi sh. bilioni 250 zinazomilikiwa na benki hiyo ambayo kwa sasa inafurahia faida ya shilingi bilioni 24 inazopata kila mwaka.
Kadhalika imefanikiwa kuanzisha huduma mbalimbali za kibenki kwa lengo la kurahisisha na kuboresha huduma kwa wateja wake huku huduma kama vile tembo kadi ,tembo kadi visa na nyinginezo.
Jambo ambalo limepanua wigo wa mtandao wa huduma hivyo wateja wao kupata huduma za kila siku hata wakiwa nje ya nchi.
SOURCE: Nipashe