WAKULIMA wawili, Makomba Reuben (32) na Said Iddy (32), jana walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa kosa la kukutwa na maganda 7,000 ya risasi.
Akisoma shitaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Neema Chusy, Mwendesha Mashitaka, Maximilian Birigi, alidai kuwa polisi wa bandari waliwahisi wakulima hao na walipowapekua waliwakuta na makasha hayo.
Washitakiwa hao walikana mashitaka hayo na walirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kulipa shilingi laki nane kila mmoja na kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi serikalini. Kesi hiyo itatajwa tena Novemba 6, mwaka huu.
Katika tukio jingine, Abdallah Musa (30), Juma Kamtile (42), mkazi wa Buguruni Malapa na Peter Liheta (30), mkazi wa Kigogo, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakituhumiwa kuiba nyaya za simu za Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) zenye thamani ya sh milioni 19.
Akisoma shitaka hilo, mbele ya Hakimu Mkazi Adolph Mahay, Mwendesha Mashitaka, Inspekta wa Polisi, Subira Tossi, alisema watuhumiwa hao waliiba nyaya hizo Oktoba 15, 2006 eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Washitakiwa wote walikana kosa na wamerudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza mashari ya dhamana waliyotakiwa kutoa hati ya nyumba na mdhamini mmoja anayefanya kazi serikalini. Kesi yao itatajwa tena Novemba 6 mwaka huu