Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Mwanafunzi kidato cha kwanza atengeneza ndege na kuirusha angani!
http://www.habaritanzania.com/articles/1493/1/Mwanafunzi-kidato-cha-kwanza-atengeneza-ndege-na-kuirusha-angani!
By Prosper Kwigize
Published on 10/24/2006
 
Mwanafunzi mwingine wilayani Kibondo amefanikiwa kukiweka hadharani kipaji chake cha ajabu baada ya kutengeneza ndege na kuirusha angani kwa mara ya kwanza na kuiacha jamii midomo wazi.

Kibondo
 
Mwanafunzi mwingine wilayani Kibondo amefanikiwa kukiweka hadharani kipaji chake cha ajabu baada ya kutengeneza ndege na kuirusha angani kwa mara ya kwanza na kuiacha jamii midomo wazi.
 
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 17 Omary Birapfumba, anayesoma kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Moyowosi wilayani hapa ameibuliwa na mwandishi wa habri hiii alipotembelea katika shule hiyo wiki hii.
 
Ndege hiyo yenye ulefu wa takribani futi tatu na upana futi moja na kimo sentimeta arobaini iliyoundwa kwa kutumia boksi na plastiki na kuwekewa vifaa kadhaa ndani pamoja na injini iliruka kimo cha karibu mita 50 juu kisha kuondoka moja kwa moja angani.
 
Wanafunzi na wafanyakazi kwa ushirikiano na walimu wa shule hiyo waliokuwepo wakati wa jaribio la kijana huyo walijaribu kwa kuirushia ndege hiyo mawe kwa nia ya kuishusha chini lakini jitihada zao ziligonga mwamba huku wakikimbia nayo mstuni.
 
Kijana Birapfumba akitumia ujuzi wa kisayansi zaidi kuliko nguvu aliwatia moyo walimu na wanafunzi wake kuwa ndege hiyo isingefika mbali kutokana na kwamba injini yake inatumia betri ndogo aina ya National Panasonic na kwamba ingeanguka chini kwa kukosa nguvu.
 
Akielezea sababu za ndege yake kuruka moja kwa moja kijana Omary Birapfumba alisema, ilitokana na hitirafu katika chombo cha kuiongozea maarufu kama rimote ambayo anaitumia katika kuongoza injini ya ndege hiyo.
 
Hata hivyo mwanafunzi huyo ambaye anadaiwa kukaa tumboni mwa mama yake kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kuzaliwa badala ya miezi tisa, amefanikiwa pia kuonesha mashine ya kufua umeme maarufu kama genereta ambayo nayo iliweza kufanya kazi.
 
Akielezea namna alivyofanikiwa kuunda chombo hicho cha usafiri ambacho ni adimu kwa watanzania kukiunda,  kijana Birapfumba alisema yeye tangu akiwa mdogo amekuwa akijishughulisha na masuala ya ubunifu.
Alifafanua kuwa licha ya kubuni na kuunga zana hizo za usafiri na uzalishaji wa umeme, tayari amefanikiwa pia kuunda mtambo wa kuvuta mawimbi ya sauti na picha za video ambapo wakazi wa kijiji cha Kifura anakoishi ambao wanamiliki runinga wameweza kupata matangazo ya ITV, Star TV, TVT na Chanel Ten.
 
Mwandishi wa habari hii anaendelea na uchunguzi zaidi ili kujua kwa undani jinsi kijana huyo alivyo fanikiwa kuunda zana hizo ikiwa ni pamoja na kuwaibua vijana wengine zaidi ambao wanavipaji ambao hawajatangazwa.
 
Hii ni mara ya pili kwa vijana wanaosoma shule za sekondari wilayani Kibondo kuunda mitambo kama hiyo baada ya kijana Eliud Kajuni aliyemaliza kidato cha nne mwaka huu katika shule ya sekondari Maragalasi wilayani Kibondo kuunda mitambo ya Radio na kufanikiwa kurusha matangazo kwa umbali wa kilomita tatu