Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Taasisi zachunguzwa kuhujumu umeme
Taasisi zachunguzwa kuhujumu umeme
By Habari Tanzania | Published  10/24/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Charles Mullinda

TAASISI mbili kubwa nchini zinazohusika kwa namna moja au nyingine na usambazaji wa nishati ya umeme kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) zinatuhumiwa kula njama za pamoja na kuhujumu mpango wa kitaifa wa kutafuta nishati mbadala ili kukabiliana na tatizo la upungufu mkubwa wa umeme nchini.

Taarifa ambazo Tanzania Daima imezinasa kutoka vyanzo vya kuaminika ndani ya serikali zinaeleza kwamba, tayari serikali imeshaanza kuzichunguza taarifa hizo, kabla hatua rasmi hazijachukuliwa dhidi ya taasisi hizo mbili (majina tunayo).

Habari zaidi zinaeleza kwamba, tayari kuwapo kwa taarifa hizo za hujuma ambazo zimeishtua serikali, zimesababisha kuzorota kwa mahusiano ya kikazi kati ya taasisi hizo mbili na viongozi wa juu wa serikali.

Kwa mujibu wa habari hizo, wasiwasi wa kuwapo kwa hujuma hizo, ulianza siku chache tu kabla hata Rais Jakaya Kikwete hajawahamisha mawaziri kadhaa, akiwamo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha ambaye sasa ni Waziri anayeshughulikia Afrika Mashariki.

Habari zaidi zinasema kwamba, eneo moja ambalo lililengwa na taasisi hizo mbili lilikuwa ni lile la kuingizwa nchini kwa majenereta yanayoendeshwa na gesi ambayo yangesaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji wa megawati 100 za umeme.

Tanzania Daima ilipowasiliana na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi jana, na kumuuliza kuhusu kuwapo kwa hujuma hizo, ikiwa ni pamoja na kumtajia majina ya taasisi zinazotuhumiwa, hakuwa tayari kukanusha wala kukubali kuhusu kuwapo kwa hali hiyo.

Hata hivyo, Karamagi alisema, serikali inakusudia kuwachukulia hatua wale wote ambao kwa namna moja au nyingine watabainika kuwa walihusika katika kukwamisha jitihada za serikali za kukabiliana na tatizo la nishati ambalo limekuwa likiongeza makali ya mgawo wa umeme nchini.

“Serikali haiwezi kusema moja kwa moja kama kuna watu waliohujumu juhudi zake za kukabiliana na tatizo la umeme, lakini ni wazi wapo watendaji ambao wamehusika ama kwa kuzembea kutekeleza majukumu yao au kwa makusudi.

“Kama mambo yalipangwa vizuri, halafu baadaye yanakwenda mrama, hilo ni kosa, hapo ni lazima serikali iwachukulie hatua kali. Sio lazima serikali itangaze hatua watakazochukuliwa moja kwa moja, zinaweza kuwa za kiutawala, lakini ni lazima wachukuliwe hatua,” alisema Waziri Karamagi.

Kauli hiyo ya Karamagi imekuja siku chache tu baada ya kutoa tamko akilaumu uamuzi wa TANESCO kuzima mitambo ya Mtera kabla hawajatoa taarifa kwake na kinyume cha taarifa waliyokuwa wamempatia awali.

Katika tamko lake hilo, Karamagi alieleza kushangazwa kwa kutopelekewa taarifa za kufungwa kwa bwawa la Mtera na kwamba taarifa aliyoipokea siku mbili kabla, ilikuwa ikieleza kuwa Mtera ilikuwa na maji ya kutosha kuendesha mtambo kwa siku 21 zaidi.

Katika hatua nyingine, Waziri Karamagi jana alilieleza gazeti hili kwamba, sehemu ya mwisho ya mitambo ya kuzalisha umeme wa megawati 20 aina ya TM 2500 inatarajiwa kuwasili nchini Ijumaa ijayo.

Alisema kuwasili kwa mitambo hiyo kutakamilisha uingizaji wa awamu ya kwanza ya mitambo hiyo inayoletwa na Kampuni ya Richmond Development ya Marekani ambayo inapaswa kuleta nchini mitambo yenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 100.

Waziri Karamagi alisema amepanga kutembelea eneo litakalofungwa mitambo hiyo wiki ijayo, ili kujiridhisha jinsi kazi hiyo inavyoendelea kabla ya kutoa taarifa rasmi kwa umma.

“Nimepata taarifa kuwa sehemu ya mwisho ya mitambo hiyo ambayo inaingizwa nchini kwa awamu, itawasili Ijumaa wiki hii, wameniambia kuwa wamelazimika kuisafirisha kwa ndege kutokana na ukubwa wa tatizo la umeme, hivyo kutumia meli ingechelewa kuwasili nchini.

“Kama ingesafirishwa kwa meli, ingekuja kamili, lakini ndege sio rahisi kwa sababu ni mikubwa. Mimi nimepanga kuwatembelea wiki ijayo ili kuona kazi ya ufungaji inaendeleaje na baada ya hapo nitakuwa katika nafasi nzuri ya kuwataarifu Watanzania kinachoendelea kuhusu suala la umeme,” alisema Waziri Karamagi.

Alisema anatarajia kuwa baada ya kuwasili kwa sehemu hiyo ya mwisho ya mitambo, kazi ya ufungaji itaanza na itakamilika katika muda uliopangwa.

Akizungumzia nyanzo vikuu vya uzalishaji umeme katika bwawa la Mtera alisema, halitarajiwi kufunguliwa mpaka mvua zitakapoanza kunyesha.

Kuhusu bwawa la Kidatu, alisema taarifa alizopokea Jumamosi iliyopita, bwawa hilo bado lina maji kidogo na linazalisha umeme wa kati ya megawati 18 na 20. Hata hivyo alieleza kuwa linaweza kufungwa wakati wowote iwapo mvua hazitanyesha.

Wakati huo huo, makali ya mgawo wa umeme ambayo yameuma kwa zaidi ya miezi mawili, yamepungua katika kipindi cha siku chache zilizopita kwa sababu ya mvua kunyesa mkoani Tanga na kuongeza uzalishaji wa umeme katika bwawa la Pangani.

Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu, Meneja Uhusiano wa TANESCO, Daniel Mshana alisema kituo cha bwawa dogo la Pangani ambacho kinahudumia gridi ya taifa kimejaa maji kutokana na mvua hizo.

“Maji yamejaa kwa wiki nzima sasa na yameongeza uzalishaji kutoka mashine moja iliyokuwa ikitumika awali hadi mashine tatu ambazo kwa jumla zinazalisha megawati 68,” alisema Mshana.

Hata hivyo, alionya kuwa kwa vile maji yanayopatikana katika bwawa hilo yanatumika yote, makali ya mgawo yanaweza kurejea wakati wowote maji yatakapopungua.
Aidha, Mshana alieleza kuwa matukio ya kukatika kwa umeme ghafla yaliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita, hayahusu mgawo wa umeme, bali matatizo ya kiufundi kwenye mfumo wa uzalishaji umeme.

“Jumamosi, gridi ya taifa ilipata hitilafu kwa saa mbili, hivyo umeme haukuwepo na katika siku hizo hizo za mwisho wa wiki, mashine zinazozalisha gesi za Songas nazo zilipata matatizo na kusababisha kukatika kwa umeme,” alisema Mshana.

Alisema mashine ya Songas iliyoharibika bado inafanyiwa matengenezo, lakini haitaathiri jitihada za TANESCO kusambaza umeme kwa wateja wake, hasa katika kipindi cha Sikukuu ya Idd.

“Katika siku hizi za Sikukuu ya Idd el Fitr, mzigo wa matumizi ya umeme kwenye mfumo wa usambazaji utapungua kwa kuwa viwanda vingi vitakuwa havifanyi kazi,” alisema Mshana


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.