MBUNGE wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, amelionya Jeshi la Polisi kuwa makini na misaada wanayopokea kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa, kwani wengine wanaweza kuitumia kama chambo cha kuvunja sheria, ikiwamo kufanya uhalifu.
Alitoa onyo hilo mwishoni mwa wiki alipokuwa akizungumza wakati wa kikao cha pamoja kati ya uongozi wa polisi mkoani Kilimanjaro na wabunge wa mkoa huo. Kikao hicho kilikuwa na lengo la kuelezea mikakati inayotekelezwa na polisi katika kukabiliana na uhalifu.
Alisema baadhi ya matajiri wanashiriki kufanya uhalifu, hivyo polisi inapoomba misaada iwe makini kwa kuhakikisha inawafahamu kwa undani, ikiwamo historia zao.
Mbunge huyo pia alilishauri jeshi hilo kujiwekea utaratibu wa kufanya ukaguzi (doria) kwenye hoteli za kitalii, kwa madai kuwa zinaweza kutumiwa na wahalifu kujificha au kupanga mikakati ya uhalifu.
“Wageni wanaofika kwenye hoteli wachunguzwe, kwani hata Wazungu wanaweza kuwa majambazi, lakini mimi kama mmiliki sitaweza kuwatambua, lazima tushirikiane ili kuwabaini watu hao,” alisema Ndesamburo ambaye pia ni mmiliki wa hoteli za kitalii za Key’s ndani na nje ya nchi.
Akijibu hoja hizo, Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Venance Tossi, alisema kuwa polisi iko makini na watu wanaojitokeza kutoa michango ya vifaa kwa ajili ya utendaji wa kazi za kipolisi, lakini hakuna ubia wowote kati ya polisi na wahisani hao.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Cyril Chami, ambaye pia ni Mbunge wa Moshi Vijijini, ambaye alishatoa msaada wa pikipiki mbili za doria kwa polisi, ameahidi kukamilisha ahadi yake kwa kuongeza pikipiki nyingine mbili mapema Februari mwakani.