Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Zanzibar yaibua minong’ono
Zanzibar yaibua minong’ono
By Habari Tanzania | Published  10/23/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu

UAMUZI wa Rais Jakaya Kikwete kupumzika Zanzibar na kufuturisha watu mbalimbali katika Ikulu ya visiwani, umeibua mawazo yenye hisia tofauti kutoka miongoni mwa wanasiasa na watu wengine.

Mbali ya hilo, taarifa kwamba, katika mapumziko yake hayo, ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema haijui madhumuni yake, Rais Kikwete alikutana na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, nayo imesababisha kuwapo kwa minong’ono mingi visiwani hapa.

Akiwa Zanzibar kwa mapumziko ya siku tano, Rais Kikwete alifikia katika Hoteli ya kimataifa ya Kempenski, iliyoko Kiwengwa, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Habari zilizopatikana zinasema kwamba, akiwa huko, Kikwete alikutana na Dk. Salmin nyumbani kwake Migombani, nje kidogo ya mji wa Zanzibar katika mazungumzo ambayo baadhi ya watu wanayahusisha na azima yake ya kupata ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la kisiasa la Zanzibar, lililovigawa visiwa vya Unguja na Pemba.

Kiongozi huyo mbali na kukutana na Dk. Salmin, mmoja wa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa visiwani na wanasiasa wengine maarufu wa Zanzibar, pia mwishoni mwa wiki aliandaa futari katika Ikulu ya Zanzibar na kuwaalika viongozi mbalimbali, wakiwamo wa madhehebu ya dini.

“Ziara hii ni hatua za kutekeleza ahadi zake, lakini jambo alilolifanya la kufuturisha Zanzibar limevunja rekodi ya viongozi wa Muungano, kwa vile ni jambo jipya,” alisema, mchambuzi mmoja wa masuala ya siasa Zanzibar.

Hata hivyo, alisema kwamba Kikwete bado ana safari ndefu ya kuleta umoja wa wananchi wa Zanzibar kutokana na kuwapo misimamo mikali ya baadhi ya wanasiasa Zanzibar.

Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais Kikwete, Maura Mwingira, alisema ziara hiyo ya Rais Kikwete ni ya mapumziko pamoja na kupata nafasi ya kufuturisha wananchi.
“Hii ni ziara ya kawaida ya mapumziko na imempa nafasi pia Rais ya kufuturisha wananchi mbalimbali”, alisema Maura.

Katibu wa Rais wa Zanzibar, Gharoub Shaibu, alisema kwamba kwa upande wao, hawafahamu madhumuni ya ziara hiyo ya siku tano.

Hata hivyo, alisema kwamba si jambo la ajabu kwa Rais Kikwete ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano kuwapo Zanzibar ambako ni sehemu mojawapo inayounda ya Jamhuri ya Muungano.

“Naomba muwatafute wasaidizi wake wanaweza kuelezea madhumuni ya ziara yake, lakini kama kiongozi wa Jamhuri ya Muungano, kuwapo Zanzibar ni jambo la kawaida,” alisema Shaibu.

Habari zinasema miongoni mwa viongozi waliohudhuria katika futari hiyo ya Kikwete, ya kwanza ya aina yake visiwani ni pamoja na Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamuhuna na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho.

Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, Amina Salum Ali, mwanasiasa wa siku nyingi Mvita Kibendera, pamoja na viongozi wa dini.

Wakizungumzia ziara ya Rais Kikwete, viongozi wa CUF walisema kwamba ina umuhimu mkubwa katika kuleta umoja wa kitaifa kwa wananchi wa visiwani.

Walisema kwamba kitendo cha kuja Zanzibar kufuturisha, kimefuta historia ya viongozi wa Muungano ambao hawakuonekana kufanya kitendo kama hicho.

“Hatua ya Rais Kikwete kufuturisha Zanzibar inaleta matumaini makubwa katika kuleta maelewano miongoni mwa wananchi wa Zanzibar,” alisema Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Bimani, msemaji wa chama hicho kikuu cha upinzani visiwani.

Kutokana na kuwapo Rais Kikwete kwa zaidi ya siku tano, wananchi wengi wamelifanya ni suala kubwa na mazungumzo katika vikao vya futari na wakati wa kunywa kahawa.

“Haiwezekani kuja kukaa muda wote huo burebure wakati ana majukumu mengi na mazito ya kitaifa, hasa wakati huu ambapo nchi inapita katika kipindi kigumu cha uhaba wa umeme,” alisema Rashid Hamad.

Katibu Mwenezi wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema ni kweli Rais Kikwete yupo Zanzibar, lakini hawezi kuelezea madhumuni ya ziara hiyo. Alishauri kuwa ni vema waandishi wa habari wakawatafuta wasaidizi wake.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.