RC Mtwara asema zinamkera na kumtia kichefuchefu
Aonya watendaji wasiobadilika atawafuta kazi bila huruma
Mhasibu halmashauri Mtwara/Mikindani Apewa miezi miwili
MKUU wa Mkoa wa Mtwara Henry Shekiffu amewaonya watendaji wakuu wa halmashauri zote mkoani mwake watakaoendelea kupata hati chafu za hesabu, watakosa kazi bila huruma.
Onyo hilo alilitoa jana wakati alipotembelea Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara, Mikindani ambapo alipata taarifa ya kazi na kuzungumza na wakuu wa idara, watumishi na madiwani ambapo alisema taarifa za hati chafu za hesabu za halmashauri zake zinamtia kichefuchefu.
Ametoa miezi mitatu kwa halmashauri hizo kukamilisha uandikaji wa vitabu vya hesabu na kumpa taarifa, na endapo kuna matatizo ya kukwamisha kazi hiyo apewe taarifa mapema ili hatua zinazohitajika zichukuliwe mara moja.
Akionyeshwa kukerwa na kwamba onyo lake siyo mzaha, mkuu huyo wa mkoa ambaye maelekezo yake hayo ya kazi yalitokana na taarifa ya kazi waliyomsomea, alimtaka Mhasibu wa Halmashauri hiyo kusafisha hesabu zake katika kipindi cha miezi miwili vinginevyo atamfukuza kazi.
“Yupo Mhasibu hapa, eenhe ni wewe ninakupa miezi miwili kusafisha hesabu zako za 2005, na kama bado itatolewa hati chafu fungasha virago uondoke,” alimweleza mweka hazina huyo ambaye naye alisema idara yake inakabiliwa na uhaba wa wafanyakazi wenye sifa zinazostahili.
Mkuu huyo wa mkoa huu ambaye huo ulikuwa mwanzo wa ziara zake za kuzitembelea halmashauri za mkoa, alisema wakurungezi ambao Mamlaka zao zitakumbwa na kuendelea kupata hati chafu wataondolewa bila msamaha wo wote.
“Wewe Mkurugenzi kama halmashauri yako itapata hati chafu ya hesabu ya mwaka uliyopita, basi ujuwe kibarua chako kimeota nyasi,” Shekiffu alimwonya mtendaji mkuu wa Manispaa hiyo na kuongeza kuwa hilo halina huruma wala msamaha kwa wakurugenzi wote.
Habari zilisema halmashauri za mkoa huo zimekuwa zikipata hati chafu kila mwaka, Manispaa ya Mtwara/Mikindani ikiwa mojawapo jambo ambalo lilimsikitisha mkuu huyo wa mkoa na kuahidi kulivalia njuga kuhakikisha mapato na matumizi ya mamlaka hizo sasa zinakuwa za uadilifu mkubwa ili kujikomboa na jinamizi la kupata hati chafu.
Alifafanua athari kubwa ya kupata hati chafu kuwa ni pamoja na kukosa ruzuku kubwa ya maendeleo inayotolewa na serikali kwa Halmashauri inayopata hati safi na kwamba yeye hatavumilia uzembe wa watendaji uwakosesha wananchi fursa hiyo ya kupata fedha hizo.
Aliwataka madiwani kusimamia kazi hizo na pia utendaji wa halmashauri zao, lakini wasibadilike na kuwa watendaji, bali zitumike sheria na kanuni katika utendaji wa kazi za kila siku na kamwe kusiachwe mwanya wa kuharibika jambo kutokana na kutotumia kanuni.
Hata hivyo, alisiifu halmashauri hiyo kwa kazi nzuri katika maeneo mengi kwa mujibu wa taarifa ya kazi aliyopewa, ingawa hakuridhishwa na baadhi ya maeneo na kusizitiza kuyafanyia kazi kwa maelekezo aliyotoa.
Kutoka gazeti la Uhuru
ISSN 0876-3896 NA.19321
Rashid Mussa, Mtwara