Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kikwete atumbukia mtegoni
Kikwete atumbukia mtegoni
By Habari Tanzania | Published  10/22/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:

IKIWA ni wiki moja tangu Rais Jakaya Kikwete afanye mabadiliko madogo katika baraza la mawaziri, uamuzi wake huo umeonekana na kuelekea kumwingiza zaidi katika mtego ambao ni vigumu kuweza kujinasua.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili na kujumuisha maoni mbalimbali yaliyokusanywa kutoka kwa wataalam mbalimbali wa siasa na utawala nchini, unaonyesha kwamba, falsafa aliyoitumia Rais Kikwete, hasa ile ya kujaribu kuwalinda wateule wake wanaoonekana dhahiri kuwa wamevurunda katika wizara zao, ni moja ya sababu kuu zitakazoendelea kumsumbua kwa muda mrefu.

Rais Kikwete anayeonekana kuwa nguzo na mhimili mkuu wa kisiasa ndani ya chama tawala (CCM), akiwa amejijengea himaya madhubuti iliyomwezesha kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka jana kwa kishindo, kukihakikishia chama hicho uhakika wa utawala wa miaka mingine mitano ijayo, anaonekana kutingwa zaidi na jinamizi lililowakuta marais wa awamu nyingine mbili zilizopita.

Kwa mujibu wa habari hizo, rais hakuwa na haraka ya kufanya mabadiliko ambayo ni ya ‘kubembelezana’ zaidi kama yalivyojionyesha, hali inayomfanya awe na deni kubwa la maelezo kwa Watanzania.

Wakati fikra hizo zikijijenga kwa upande mmoja, upande mwingine unasema kuwa Kikwete amekosea kwa kujaribu kuulea au kuukingia kifua uzembe, hali ambayo itamsumbua hata atakapofikiria kufanya mabadiliko mengine ya uhakika.

Hali hiyo, kwa vyovyote vile na kwa mujibu wa wataalam hao ndiyo inayoelezea namna ambavyo atapata ugumu wa kuendesha serikali yake kwa kipindi kingine kijacho na hivyo kivuli chake kitamsumbua. Mtaalam mmoja anaeleza kwamba kwa mfano, Rais Kikwete alipaswa kuwaondoa ofisini baadhi ya mawaziri ambao bila shaka anaamini kwa dhati kwamba walisababisha matatizo katika utendaji wa wizara zao.

Ingawa, bila kumtaja au kumhusisha moja kwa moja, lakini anatajwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Dk Ibrahim Msabaha. Kubwa, linaloonekana kumfuata Dk Msabaha hata kama amehamishwa ni mbinu zake za kuweza kukabiliana na kumaliza tatizo sugu la mgawo wa nishati ya umeme.

Upande huo, unasema kuwa Rais Kikwete alifanya mabadiliko hayo wakati suala hilo la mgawo huo wa umeme likiwa halina dawa na mgawo huo ukiongezeka badala ya kupungua, huku kukiwa na dhana kwamba suala la upendeleo katika ugawaji wa rasilimali ya taifa likiongezeka, na mengineyo kadhaa.

Mwanasiasa wa siku nyingi na Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Makani kwa upande wake, akizungumza katika mahojiano maalum na Mwananchi Jumapili alisema endapo Rais Kikwete anataka kuleta mabadiliko ya kweli aliyowaahidi Watanzania, basi hana budi kuteua watu wenye uwezo kuongoza nchi badala ya kuegemea kigezo cha uanamtandao.

“Kosa kubwa alilolifanya rais na hili litaendelea kumsumbua ni kuwateua wanamtandao wake bila kujali uzoefu, ujuzi na background (historia) yao,” alisema. Mwanasiasa huyu anasema tatizo la wanamtandao bado linaendelea kumsumbua Rais Kikwete na serikali yake kwa kuwa wengi wa watu aliowateua kushika nyadhifa za uwaziri na unaibu waziri ni watu wake wa karibu.

Anasema kutokana na kuogopa kivuli cha wanamtandao hao kwa kuzingatia kuwa kipo kibarua kingine cha uchaguzi mkuu mwaka 2010, Kikwete ameshindwa kufanya maamuzi ya kuwafukuza baadhi ya watu wake wa karibu licha ya kuonekana dhahiri kuboronga katika wizara zao.

“Hayupo tayari kwa hilo, ukizingatia watu wake hao anawategemea sana kwenye kinyang’anyiro kijacho cha Uchaguzi Mkuu (2010),” alisisitiza Sambamba na hilo, mwanasiasa huyo mkongwe anasema si vyema kwa rais kufanya mabadiliko makubwa kama hayo tena baada ya miezi 10 tu tangu aingie madarakani.

“Tuko kwenye zama za uwazi na ukweli, hivyo rais hana budi kutueleza sababu hasa iliyomlazimu kuchukua uamuzi huo.” Makani alisema kitendo cha Rais Kikwete kuwabadilishia wizara mawaziri na manaibu mawaziri pia kinaleta maswali kwani baadhi alipaswa kuwaondoa. “Anaendeleza mtindo wa CCM wa unakosea hapa unapelekwa kule….. nchi haijengwi namna hiyo, Rais anapaswa kuwa mkali.”

Bila kuwataja majina, Makani alisema Rais Kikwete alipaswa kuwaondoa baadhi ya mawaziri na manaibu wao kwa kile alichodai kuwa waliboronga kwenye wizara zao za zamani. Badala yake, anasema Rais Kikwete amewapaka mafuta kwa mgongo wa chupa wananchi kwa kuwabadilishia wizara mawaziri hao bila ya kujali kuwa wananchi wanapata tabu. Alisema baadhi ya mawaziri wamekuwepo kwenye uongozi wa nchi tangu serikali ya awamu ya kwanza.

Naye, msomi, mwanasayansi na Mwenyekiti wa chama cha siasa cha Demokrasia Makini, Profesa Leonard Shayo anahoji sababu za kitendawili hiki cha kubadilishwa kwa mawaziri.

Anaeleza kuwa viongozi wa kisiasa wanaoshindwa kuongoza eneo moja, halafu wanapewa eneo lingine, wanaipeleka pabaya Tanzania. Anakiri kwamba waziri ni kiongozi wa kisiasa, anayetakiwa ahakikishe kwamba, wataalam wa wizara yake wanatekeleza sera za chama tawala, lakini, anahoji waziri anayeshindwa kutumia wataalam wa wizara moja kufanikisha hilo, atawezaje kutumia wataalam wa wizara nyingine?

Anapendekeza mfumo wa kubadilisha baraza la mawaziri kwa kubadilishana ofisi, badala ya kuteua wapya, utazamwe upya na kushauri kuwa kazi ya waziri ni kuhakikisha utekelezaji wa sera za chama tawala, kuyumba kwa wizara ni matokeo ya kushindwa kuwatumia vema wataalam.

Pamoja na ushauri na misimamo kama hiyo, habari ambazo Mwananchi Jumapili inazo, zinaeleza kuwa, uamuzi wa Rais Kikwete kutumia staili hiyo ya uwajibishaji kama turufu katika kuongeza kasi yake ya utendaji imetokana na tafakari aliyoifanya akiwa Mwenyekiti wa Chama cha CCM kwa kuzingatia hali halisi ya chama.

Miongoni mwa mawaziri ambao wanasemekana kumuingiza Rais mtegoni na ambaye amekuwa majeruhi wa hamisha hamisha hiyo na ambaye amekuwa akitajwa hasa kutokana na sakata la Kampuni ya Richmond Development Company ya Marekani (ambayo baada ya kelele nyingi imeingiza majenereta ya umeme nchini jana).

Ingawa alipata mafanikio makubwa katika miezi ya awali ya utawala wake na hivyo kukijengea uhalali CCM, kwa kupunguza uhalifu kwa kiasi kikubwa, matamko yake kuhusu suala la biashara ya samaki (mapanki) na hili sasa la nishati, vinaanza kuibua maswali mengi kwa wananchi.

Hata hivyo, kama mambo yataenda bila ya kubadilika, Kikwete anaweza akajinasua katika mtego huo akitumia busara zaidi, iwapo kundi la wanamtandao ambalo yeye alikuwa mmojawapo halitamwangusha na kufanya kazi kadiri inavyotakiwa.

Mathew Kwembe na Yahya Charahani Mwisho


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Dr, Nicholas Gregory)
    Rating
    The article is poorly researched. It has inadequate data, and its allegations as per title are nowhere substantiated. This just another rumbling mixture of rumour, hearsay and pure juvenile excitement about a serious allegation.
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.