Na Merali Chawe, Mbeya
ZAIDI ya wateja 300 wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) mkoani hapa wamekuwa wakikosa mawasiliano ya simu kwa nyakati tofauti kuanzia Machi hadi Oktoba mwaka huu na kuisababishia kampuni hiyo hasara ya zaidi ya Sh1 bilioni kutokana na wizi wa nyaya za simu na mikonga.
Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, Suleiman Kova alisema juzi kuwa kufuatia wizi huo, watu 18 wanashikiliwa na jeshi hilo na baadhi yao wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.
Kamanda Kova alisema kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na maafisa wa TTCL kutoka makao makuu ya kampuni hiyo jijini Dar es salaam walifanikiwa kukamata tani saba za nyaya za simu zilizokutwa kwenye maghala ya kuhifadhia vyuma chakavu.
Kamanda Kova aliyataja maeneo yaliyokumbwa na wizi wa nyaya na mikonga ya simu kuwa ni Uyole,Mbalizi-Songwe,Mbalizi-Utengule, Iyunga,Runje Farm, Mwanjelwa,Igogwe, Kibisi-Kyimo, Rungwe Mission, Sekondari ya Rungwe, Magereza na Chuo cha Barabara Rungwe.
Alisema kwamba kutokana na biashara ya shaba imesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu nchini hasa katika mashirika mama kama vile TTCL, Shirika la Umeme la Tanzania, (Tanesco) Shirika la Reli Tanzania (TRC) na ile ya Tanzania na Zambia (Tazara).
Kamanda Kova alisema kwamba kwa wale watakaosaidia kutoa taarifa na kufanikisha kukamata wezi wa nyaya za simu watazawadiwa Sh300,000 na kuwaomba wananchi washirikiane na jeshi hilo kwa kutoa taarifa