Na Mussa Juma, Arusha
WAFANYABIASHARA wa madini ya tanzanite wanatarajia kuanza kunufaika na soko kubwa la madini hayo nchini Marekani kufuatia mwakilishi wa kampuni kubwa ya ununuzi wa vito ya nchi hiyo,Tiffany kuridhishwa na kazi za wachimbaji hao.
Akizungumza na wachimbaji hao, aliyekuwa mratibu wa safari ya wafanyabiashara walioandamana na Rais Jakaya Kikwete nchini Marekani mwezi huu, Richard Kasesera alisema kutokana na ujio wa mwakilishi wa kampuni hiyo, kutakuwa na mabadiliko makubwa katika biashara ya madini hapa nchini.
Kasesera alisema wakiwa Marekani wakati wa ziara hiyo, walikutana na Rais wa kampuni hiyo ya Tiffany ambaye aliahidi kumtuma mwakilishi wake kuja nchini na kuona jinsi ya upatikanaji wa madini hayo na mazingira ya uchimbaji.
"Kwa jinsi nilivyomuona mwakilishi wa kampuni hii, Marcelo Souza ni wazi ameridhika na mazingira ya uchimbaji na jinsi wachimbaji wadogo wanavyofanyakazi zao"alisema Kasesera.
Alisema mwakilishi huyo wa Tiffany alitembekea ofisi za wachimbaji wadogo na wakubwa wa Tanzanite One na pia alitembelea mgodi wa Rahim Massawe uliopo eneo la kitalu D ambao uliusifia sana.
Akiwa katika mgodi huo wa Massawe, Souza alitembelea eneo linalochimbwa madini na kuzama chini, vyumba vya kulala wachimbaji wadogo na sehemu ya burudani wanapopumzika.
Wakizungumza na mwakilishi huyo, Mkurugenzi wa Prima Gems, Hussein Gonga na mchimbaji, Rahim Massawe walimpongeza kwa kutembelea maeneo yao.Gonga ambaye naye alitembelea kampuni hiyo nchini, Marekani alisema ana uhakika watafanya nayo biashara hasa baada ya mwakilishi huyo kueleza kuridhishwa na kazi zao.
Wachimbaji hao, walipongeza pia Rais Kikwete kwa jitihada zake za kuwatafutia masoko ya madini yao hasa baada ya kwenda nao Marekani ambako walitembelea makampuni kadhaa ambayo yananunua madini ya aina mbali mbali.