Na Ramadhan Semtawa
TUME ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) imeutua mzigo kwa kueleza kwamba imemaliza jukumu lake katika mchakato wa kuipata menejimenti mpya ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na kuwasilisha ripoti yake Wizara ya Miundombinu.
Kwa muda mrefu, pande hizo mbili zimekuwa zikitupiana mpira, baada ya Wizara ya Miundombinu kudai kuwa PSRC ndiyo haijamaliza kazi yake ya kuitathmini Kampuni ya Saskatel International ya Canada kupitia Kamati ya Ufundi (Technical Committee) na kisha kuwasilisha ripoti yake wizarani hapo.
Katika kamati hiyo ya ufundi ambayo ilikuwa chini ya PSRC, miongoni mwa mambo ambayo ilifanya ni kuangalia uwezo wa kiutendaji wa Saskatel International, mtaji wake na mafanikio iliyopata katika utendaji wake.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili jijini Dar es Salaam juzi, Afisa Habari Mwandamizi wa PSRC, Joseph Mapunda, alisema tayari tume hiyo imekwishawasilisha ripoti wizarani.
Mapunda alisema kamati ya ufundi imekamilisha ripoti hiyo baada ya kutekeleza majukumu yake ya msingi iliyokuwa imepewa.
"Ripoti tayari iko wizarani, kamati imekwishamaliza kazi yake, kwa hiyo taarifa za maamuzi zinapaswa kutolewa na wizara," alieleza Mapunda.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Omary Chambo, alipoulizwa kuhusu lini hasa menejimenti ya Saskatel International ya Canada itaanza kazi baada ya PSRC kuwasilisha ripoti yake alijibu: " Suala hilo kwa sasa lipo chini ya Katibu Mkuu (John Kijazi)."
"Yeye ndiye anayeweza kulizungumzia vizuri kwani ndiye anayesimamia mchakato wa wizara wa kuipata menejimenti ya TTCL, mimi kwa kweli sina taarifa za kutosha," alisema Chambo.
Alipotafutwa kwa simu, Kijazi hakupatikana kuzungumzia suala hilo.
Kampuni ya Saskatel International ilipaswa kuanza uongozi wa menejimenti ya TTCL tangu Mei baada ya kushinda zabuni iliyotangazwa na PSRC, Januari.
Hata hivyo, hadi sasa ikiwa ni miezi karibu sita, Saskatel International haijaweza kuanza kazi rasmi, lakini taarifa zaidi zikisema serikali imekuwa makini katika kuikabidhi menejimenti ya TTCL kwa kampuni hiyo kwa kuhofu yaliyotokea kwenye kampuni nyingine MSI/Detecon (Celtel International).
Katika mkataba wa MSI/Detecon wa mwaka 2001, serikali ilijikuta ikiingia katika mvutano na kampuni hiyo baada ya kukataa kulipa salio la dola 60 milioni zilizosalia badala yake ikalipa wastani wa dola 4.5 milioni kukiwa na mvutano kati ya menejimenti hiyo na wafanyakazi hali iliyosababisha uendeshaji TTCL kudorora katika kipindi chote cha miaka minne