Muhibu Said na Mkinga Mkinga
KAMPUNI ya Kimarekani ya Richmond Development (RDC), hatimaye imeingiza nchini majenereta ya kufua megawati 100 za umeme na kuondoa minogong'ono iliyozagaa iwapo kampuni hiyo ni ya kweli au ya ulaghai wa kibiashara.
Shehena hiyo ya kwanza ya mtambo wa kuzalishia umeme iliwasili nchini huku Meneja Mkazi wa RDC nchini, Naeem Gire akieleza kuwa shutuma dhidi ya kampuni yake zina mkono wa siasa.Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, alisema shutuma zilizoelekezwa RDC na baadhi ya watu kuhusu mtambo huo, zilitokana zaidi na msukumo wa kisiasa na chuki za kibiashara, kinyume na ukweli.
Alisema wao wanavyo vielelezo vya uhakika vinavyothibitisha kwamba RDC ni kampuni halali iliyosajiliwa kisheria katika mji wa Houston, Jimbo la Texas, Marekani na pia imepitia taratibu zote za uwekezaji katika Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC).Alisema mbali na hayo, mkataba wa kuingiza mtambo huo, ulitiwa saini na pande zinazohusika kwa njia za wazi na mbele ya baadhi ya viongozi wakuu wa serikali na wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), wakiongozwa na Waziri wa Nishati na Madini.
Alisema baadhi ya viongozi wa serikali na Tanesco (hawataji) wanaufahamu vema ukweli huo na kwamba, waliwahi hata kufika pia Marekani na kujionea kwa macho yao mipango ya maandalizi ya usafirishwaji wa mtambo huo kuletwa nchini.
Alisema kinyume na ukweli huo, kinachoonekana nyuma ya shutuma zilizoelekezwa kwa kampuni yake, ni chuki za kisiasa na biashara zinazoendeshwa na baadhi ya watu baada ya kushindwa katika kinyang'anyiro cha kupata zabuni hiyo iliyotangazwa kimataifa.
"Suala hili limekuwa likichukuliwa kisiasa zaidi na watu ambao waliomba zabuni hii na kisha kuikosa. Sasa, leo (jana) tunadhihirisha kwa vitendo dhidi ya kile tulichokuwa tunashutumiwa kwa maneno," alisema Gire.Alisema watu hao wameshindwa hata kufahamu muda wa mkataba uliofikiwa kati ya kampuni yake na Tanesco wa kuingiza na kufunga mtambo huo nchini.Alisema kinyume na madai ya watu hao kwamba RDC, haikuwa kampuni ya kweli na ndio maana siku ambazo mtambo uliahidiwa kufungwa kuisha bila kufungwa, katika mkataba huo walikubaliana na Tanesco kuingiza na kuufunga mtambo huo ndani ya siku 60, kuanzia Septemba 18 hadi Novemba 18, mwaka huu.
"Shutuma hizo zimetuumiza sana kwa sababu hata mimi kila nikipita mjini naambiwa mwizi, ndiye Richmond mwenyewe huyu," alisema Gire.Hata hivyo, alisema hawawezi kuchukua hatua zozote dhidi ya watu waliokuwa wakitoa shutuma hizo na badala yake wanachokusdia kuuonyesha umma wa Watanzania, ni kufanya kazi iliyokusudiwa.Alisema madai kwamba, fedha zilizotumika kununulia mtambo huo zimekopwa kutoka mashirika ya fedha ya kimataifa, hayana ukweli wowote na kwamba, fedha hizo zinatoka kwenye kampuni hiyo ambayo alisema anaimiliki yeye na kaka yake, Mohamed Gire, anayeishi , Houston, Marekani. Alisema kuwa ni kweli kwamba anafanya biashara ya internet, lakini akawashangaa watu wanaohoji uwezekano wa mfanyabiashara anayetoa huduma hiyo kuingia mkataba mkubwa kama huo wa kufunga mtambo wa kuzalisha umeme.
"Mbona wapo wafanyabiashara wakubwa hapa nchini ambao wanafanya biashara ya kuuza maji ya mifuko ya plastiki ?," alihoji Gire.Sehemu ya mtambo huo, uliwasili nchini saa 3:00 asubuhi kwa ndege ya kukodi aina ya Antonov inayomilikiwa na Kampuni ya VOLGA DNEPR ya Russia ikiongozwa na wahandisi wa Kimarekani.Gire alisema sehemu ya mtambo iliyowasili, itaanza kufungwa haraka iwezekanavyo mapema wiki ijayo. Kazi hiyo itafanywa na mhandisi wa kampuni hiyo kutoka Marekani, Goldon Ware na kwamba, sehemu iliyobaki, itawasili nchini siku yoyote kuanzia Jumatano wiki ijayo.Alisema imeshindikana kusafirisha kwa pamoja sehemu zote za mtambo kutokana na ukubwa, uzito na aina ya mtambo huo na ugumu wa upatikanaji wa ndege ya kuusafirisha.
Gire, alisema mtambo huo ujulikanao kama "Exhaust Inlet Auxilliary Machine" utakaofungwa katika Kituo cha Ubungo, jijini Dar es Salaam, utakuwa na uwezo wa kufua umeme wa kiwango cha megawati 22.8, lakini kutokana na hali ya hewa ya Tanzania, alisema unaweza kutoa megawati kati ya 21 na 20.Hata hivyo, alisema ni mapema kutaja gharama halisi zilizotumika kuununua na kwamba, suala hilo litajulikana mara baada ya sehemu yake iliyobaki itakapowasili nchini.Juzi, RDC ilitoa taarifa katika vyombo vya habari ikieleza kuwa mitambo yake ilikuwa ikitarajiwa kuwasili Dar es Salaam kwa ndege jana.