MVUTANO mkubwa umeibuka ndani ya kikao cha Baraza la Wawakilishi baada ya Waziri Kivuli wa Wanawake na Watoto, Zakhia Omar, kushauri watu wanaoingia kutoka nje ya Zanzibar kupima afya zao ili kufanikisha kampeni dhidi ya UKIMWI.
Mwakilishi huyo alisema hayo wakati akichangia Sera ya Ukimwi Zanzibar iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Kiongozi, Amina Salum Ali.
Waziri Kivuli huyo alisema kwamba iwapo serikali itaweka udhibiti wa kuwapima afya zao watu wanaoingia kutoka nje ya Zanzibar itasaidia kupunguza kasi ya maambukizi kwa vile wataweza kufahamika na kurejeshwa walikotoka.
Alisema yako mataifa mengi yenye utaratibu wa kukagua afya za watu wanaoingia katika nchi hizo kabla ya kuruhusiwa kuingia.
“Mheshimwa Spika, lazima kuwepo na udhibiti wa uingiaji watu Zanzibar ili kudhibiti maambukizi mapya ya UKIMWI Zanzibar,” alisema.
Mchango huo ulionekana kuwagusa viongozi wa serikali, akiwamo Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, na Waziri Amina Salum Ali, ambao walipinga ushauri huo.
Akichangia Sera hiyo, Waziri Kiongozi alisema ni vigumu kudhibiti watu wanaoingia Zanzibar hasa kwa kuzingatia kuwa na Wazanzibari wanatoka na kwenda kuishi nje ya Zanzibar.
“Ni vigumu kudhibiti uingiaji wa watu ndani ya Zanzibar kwa sababu watu wa Zanzibar nao wanatoka nje, sasa wanaporudi tutakuwa na uhakika gani kuwa nao wako salama?” alihoji Waziri Kiongozi.
Alisema kwamba, njia pekee ya kuepuka UKIMWI ni kuacha vitendo vya zinaa na kwa wale wakaidi, watumie njia zitakazowanusuru na maambukizi hayo.
Aidha, Waziri Kiongozi amewataka madaktari kuacha tabia ya kutoa siri za watu wanaopima UKIMWI, kwa vile ni kinyume cha maadili ya kazi zao na kutaka watu wapimwe UKIMWI kwa hiari zao.
Mapema Mwakilishi wa Jimbo la Ole, Hamad Masoud, alisema lazima iwepo sheria ya watu kupima UKIMWI kabla ya kufunga ndoa. Alisema hiyo ndiyo njia muafaka itakayosaidia kupunguza kasi ya maambukizi ya UKIMWI.
Akifunga mjadala huo, Waziri Amina Salum Ali, naye alisema, si muafaka kuanza kuwapima UKIMWI watu wanaoingia Zanzibar kwa vile wapo Wazanzibari wengi wanaokwenda kufanya kazi katika mikoa ya Tanzania Bara.
Alieleza kwamba, wapo Wazanzibari wanaoendesha shughuli zao katika sehemu mbali mbali ya Tanzania Bara na kuitaja kwa mfano Tunduma (Mbeya) na Dodoma. Wengine wanaishi Shimoni, Kenya na hata Somalia.
Waziri huyo alisema kwamba tatizo lililopo Zanzibar ni unyanyapaa kwa watu waliokwisha athirika kwa UKIMWI, na zaidi kisiwani Pemba.
Alisema kwamba kisiwani Pemba wagonjwa wengi wa UKIMWI wananyanyapaliwa na jamii, vitendo ambavyo ni kinyume cha haki za binadamu, kwa vile watu walioathirika kwa maradhi hayo wana haki sawa na watu wengine.
Aidha, alisema serikali imegundua idadi kubwa ya watu Pemba walioathirika kwa ugonjwa huo wamekuwa wakikimbia dawa za kurefusha maisha (ARV).
Alisema kwamba lengo la kuanzishwa sera hiyo ni kuanzisha utaratibu mzuri katika kupiga vita UKIMWI.
Mapema Mwakilishi wa Viti Maalumu (Walemavu), Raya Suleiman Hamad alisema amepokea barua kutoka kwa Jumuiya za Walemavu wakiwalaani wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (CUF) kwa kutokuunga mkono muswada wa kuongeza fursa na haki kwa watu wenye ulemavu.
Akichangia sera hiyo, alisema kwamba, kitendo cha wajumbe wa CUF kutounga mkono muswada huo kimewavunja moyo katika juhudi za uimarishaji wa ustawi wa watu wenye ulemavu kwa vile sheria hiyo imelenga kuwaondolea matatizo yanayowakabili hivi sasa.