Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mtanzania mwingine afa kiutatanishi Uingereza
Mtanzania mwingine afa kiutatanishi Uingereza
By Habari Tanzania | Published  10/21/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Mwandishi Wetu

MTANZANIA mwingine amepoteza maisha yake kwa kuteketea kwa moto wakati akiwa nyumbani kwake London, nchini Uingereza, katika mazingira ambayo taarifa za awali zinaonyesha kuwa mauaji hayo ni ya kupangwa.

Habari ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka London na kutoka kwa ndugu na jamaa wa karibu wa marehemu aliyetajwa kwa jina la Fatuma Kashuma (35), mwenye asili ya Mkoa wa Kilimanjaro, zinaeleza kwamba, tukio hilo ambalo hadi sasa linaendelea kuchunguzwa na vyombo vya dola nchini Uingereza lilitokea hivi karibuni.

Watu wanaomfahamu Fatuma na ambao wako karibu na familia ya Kashuma waliieleza Tanzania Daima kwamba, mwanamke huyo mwenye mtoto mmoja alifikwa na mauti hayo wakati akiwa nyumbani kwake huko London alikokwenda kwa shughuli za masomo.

Fatuma ambaye kabla ya kuondoka nchini kwenda London alikuwa akifanya kazi katika Shirika la kimataifa la misaada la Care International katika maeneo ya wakimbizi, Ngara na baadaye Kigoma, aliondoka nchini mwaka 1999 baada ya mkataba wake wa kazi kumalizika mwaka mmoja kabla.

Habari zinaeleza kwamba, mara ya mwisho, Fatuma alikuwa hapa nchini miezi takriban mitatu tu iliyopita alipofika kuhudhuria mazishi ya baba yake mzazi aliyefariki dunia siku zipatazo 52 kabla ya yeye mwenyewe kufariki dunia.

Mtu mmoja aliye karibu na familia ya kashuma aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina gazetini alisema, wakati akiwa Ngara, Fatuma alikutana na mwanamume wa Kijapani waliyekuja kufunga naye ndoa na baadaye wakafanikiwa kupata mtoto mmoja.

Miaka kadhaa baadaye, mwanamume huyo wa Kijapani mwenye jina la Yuji Kaketomo, ambaye awali alikuwa mfanyakazi wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), hapa nchini, alipata kazi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na akapangiwa kufanya kazi nchini Irak.

Kaketomo alipopata kazi Irak, mkewe alibakia Dubai alikokuwa akiishi kabla hajapata nafasi ya masomo ambayo ilimpeleka London, Uingereza, alikokwenda masomoni na akawa akiishi hadi mauti yalipomfika hivi karibuni.

Habari ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka London zinaeleza kwamba, akiwa Uingereza, Fatuma alikutana na kijana mmoja wa Kitanzania ambaye walikuwa wakifahamiana kwa miaka mingi kabla.

Kwa mujibu wa habari hizo, hadi alipopatwa na mauti hayo, Fatuma na kijana huyo wa Kitanzania ambaye ni mtoto wa ofisa mmoja wa juu katika shirika moja la umma (jina tunalo), walikuwa watu waliokuwa na mahusiano ya karibu, ambayo baadhi ya watu waliowafahamu walikuwa wakiyahusisha na kuwapo kwa mahaba baina yao.

“Unajua inasemekana kuwa hawa watu wawili, Fatuma na ...(kijana huyo wa Kitanzania) walifikia hatua ya kufunga ndoa na kuishi pamoja kama mume na mke, ingawa Fatuma hakupata kumweleza mwenzake kuwa tayari alikuwa na mume mwingine ambaye ndiye waliyezaa naye mtoto,” kilisema chanzo chetu kimoja cha habari.

Kwa mujibu wa chanzo hicho cha habari, kitendo cha Fatuma kutomweleza mwanamume huyo ukweli kuhusu ndoa yake na mwanamume mwingine, ndicho kinachohofiwa kuwa kichocheo cha kifo chake.

“Taarifa tulizonazo zinaeleza kwamba, huyo kijana baada ya kukaa kwa muda mrefu na Fatuma hatimaye alibaini ukweli wote kuhusu ndoa ya awali ya mwenzi wake na kijana huyo wa Kijapani, hali ambayo hatimaye ilisababisha aamue kulipiza kisasi kwa kumuua,” kilisema chanzo kingine cha habari hizo.

Tanzania Daima iliwasiliana na dada wa marehemu ajulikanaye kwa jina la Asha Kashuma, aliyepo hapa nchini ili kupata habari zaidi kuhusu kifo hicho cha ndugu yake na taarifa walizonazo hadi hivi sasa.

Akizungumza kwa uchungu, Asha alisema wao bado wanaendelea kusubiri taarifa za kipolisi kuhusu sababu hasa za kifo cha ndugu yao na kwamba, kwa sasa hawawezi kueleza lolote zaidi ya kuusubiri mwili wa marehemu unaotarajiwa kuwasili nchini wakati wowote kuanzia sasa.

“Sisi tunachojua ni kwamba sababu za kifo chake ni moto, hatuna zaidi ya hilo. Kwa sasa siwezi kueleza lolote kwani kusema jambo lolote kunaweza kukasababisha nikaanza kulia tena sasa, tusubiri taarifa ya polisi kwanza ndipo nitakapokuwa tayari kueleza,” alisema Asha.

Aidha, ndugu huyo wa marehemu alilieleza gazeti hili kwamba, ndugu yao mmoja ambaye hakumtaja jina, anayefanya kazi Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa ndiye anayefuatilia taratibu zote za kuusafirisha mwili wa marehemu hadi hapa nchini.

Pamoja na Asha kukiri kwamba mazishi ya ndugu yake huyo yatafanyika hapa na kutokuwa tayari kuingia katika undani wa suala hilo, habari kutoka kwa ndugu wengine wa karibu zinasema kwamba, mwili wa marehemu unatarajiwa kufika hapa na kuzikwa Novemba 9, mwaka huu.

Kifo hicho cha Fatuma kimetokea wakati Watanzania wakiwa na kumbukumbu ya msiba mwingine uliowakuta vijana wengine wa Kitanzania Detroit, Marekani, uliotokea Septemba 20.

Vijana hao wachumba, Walter Mazula (28) na Vonetha Nkya (28), waliuawa na watu wasiojulikana wakati wakienda kazini katika mazingira ambayo bado yamebakia kuwa kitendawili kilichokosa mteguzi.

Wakati maiti ya Walter iliokotwa meta chache kutoka katika gari walilokuwa wakitumia, ikiwa na matundu ya risasi, ile ya Vonetha ilikutwa ndani ya gari hilo ambalo liliteketezwa kwa moto na wauaji hao


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.