Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kabourou: Sibebwi na Makamba
Kabourou: Sibebwi na Makamba
By Habari Tanzania | Published  10/20/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Kulwa Karedia

ALIYEKUWA Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Aman Kabourou, amesema hajabebwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, tangu alipojiunga na chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye ukumbi mdogo wa Bunge, Dar es Salaam, Kabourou amekanusha habari kuwa tangu amejiunga na chama hicho mwanzoni mwa Septemba, amekuwa akibebwa na Makamba, ili kupata umaarufu wa haraka ndani ya chama hicho.

“Siyo kweli kwamba mimi nabebwa na Makamba tangu nimejiunga na CCM kutoka Chadema. Nina uwezo mkubwa na sera zangu zinakubalika, na hii ndiyo silaha yangu katika masuala ya siasa,” alisema Kabourou.

Alisema kutokana na uwezo wake katika masuala ya siasa ana uhakika wa kushinda katika uchaguzi ujao wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki endapo akiteuliwa na chama chake katika hatua ya mchujo utakaofanyika Dodoma mapema mwezi ujao.

“Naamini kama nikipitishwa na chama changu katika uchaguzi ujao wa Bunge la Afrika Mashariki kwenye mchujo wa chama kule Dodoma, nina hakika naweza kushinda katika uchaguzi huo ambao unaonekana kuwa na wagombea wengi,” alisema Kabourou.

Alisema lengo la kuwania nafasi hiyo ni kutaka kutoa mchango kwa wananchi wa Afrika Mashariki, katika nyanja mbalimbali zikiwamo za uwekezaji na masoko, hali itakayosaidia wafanyabiashara wa nchi hizo.

Alisema siasa za Tanzania zinaonyesha wazi kuwa wananchi wengi wana imani kubwa na CCM kutokana na sera zake kukubalika, pia kutekeleza vizuri ilani yake ya uchaguzi, tofauti na vyama vya upinzani ambavyo siku zote vimekuwa na kazi ya kukosoa.

“Niliamua kujiunga na chama chenye serikali, kwani kimekuwa makini katika kutatua baadhi ya kero zinazojitokeza. Sasa kule upinzani kila siku ni ukosoaji tu,” alisema Kabourou.

Alisema viongozi wengi walioko nje ya CCM, wamekuwa mabingwa wa kupiga kelele ambazo hazizai matunda kwa wananchi ambao ndiyo nguzo kuu.

Alisema siku zote ambazo amekuwa kambi ya upinzani alishindwa kushiriki kikamilifu katika suala zima la uundaji wa sera mbalimbali za serikali.

“Nawashauri viongozi wa vyama vya upinzani kujiunga na CCM, kwani siyo chama chenye wazo moja kama wanavyofikiria wao, hiki ni chama chenye watu wenye mawazo mengi,” alisema Kabourou.

Akitoa mfano, Kabourou alisema hakuna kiongozi yeyote wa kambi ya upinzani ambaye amewahi kuandika kitabu kuelezea hali halisi ya Watanzania, tofauti na aliyekuwa Mbunge wa Ilala, Idd Simba, aliyeandika kitabu kuhusu wazawa.

“Sijawahi kuona kiongozi wa upinzani kaandika kitabu kuelezea hali ya Watanzania, ni mtu mmoja, Idd Simba, aliyekuwa mbunge wa Ilala, aliandika kuhusu wazawa, sasa hii inaonyesha mtu aliye makini (serious) anapaswa kujiuliza,” alisema Kabourou.

Kabourou alijiunga na CCM mwezi uliopita akitokea Chadema, ambako alikuwa mmoja wa viongozi wenye nguvu katika kambi ya upinzani.

Wakati huo huo, kampeni za chini chini zimeanza kushika kasi kutokana na wengi wa wagombea kupita huku na huko kwa wabunge, kwa lengo la kujinadi.

Hali hiyo ilijionyesha wazi jana baada ya Tanzania Daima kushuhudia wagombea (majina tunayo) wakipita huku na huko kwa wabunge wanaohudhuria vikao mbalimbali vya kamati za Bunge.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.