WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wa kambi ya upinzani kutoka CUF wamesema Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), ndiyo kikwazo kikubwa katika kuinua uchumi wa Zanzibar.
Walisema hayo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea Zanzibar, wakati wakijadili sera ya viwanda na biashara, iliyowasilishwa na Waziri wa Utalii, Biashara ya Uwekezaji, Samia Suluhu Hassan.
Mwakilishi wa Viti Maalumu, Zahara Hamad amesema kwamba tangu Zanzibar kuingia katika mfumo wa viwango sawa vya kodi baina ya Bara na Zanzibar, sekta ya biashara Zanzibar imekuwa ikiporomoka kwa kasi.
“TRA imekuwa ikiua biashara za Wazanzibari na sasa wamekuwa hawafanyi tena biashara za kuchukua mizigo Bangkok na Dubai,” alisema mwakilishi huyo.
Alisema kwamba wataalamu wa kodi wa TRA waliamua kuweka viwango sawa vya kodi kati ya Bara na Zanzibar bila ya kuzingatia mazingira ya kibiashara kati ya pande hizo.
Hata hivyo, mwakilishi huyo aliilaumu Serikali ya Zanzibar kwa kutokuwa na sera nzuri ya kulinda viwanda vya ndani, na kusababisha viwanda vyote kufa, vikiwamo vile vilivyoanzishwa na Rais wa Kwanza, marehemu mzee Abeid Aman Karume.
Alisema kwamba Wazanzibari ‘si wavivu’, isipokuwa sera za uendelezaji viwanda na biashara hazisimamiwi vizuri na watendaji.
Akichangia sera hiyo, Mwakilishi wa Ziwani (CUF), Rashid Seif Suleiman alisema kwamba matatizo ya Zanzibar ya kiuchumi yanatengenezwa na Benki Kuu.
Alisema kwamba majukumu makubwa ya benki hiyo ni kulinda uchumi wa serikali zote mbili, lakini ni ajabu Zanzibar inaingizwa katika mfumo wa kodi ambao utaathiri uchumi wake.
Mwakilishi huyo alisema kwamba iwapo BoT ingetimiza wajibu wake, Zanzibar haiwezi kuingizwa katika mfuko kama huo wa kodi wakati kuna tofauti kubwa ya kiuchumi kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.
Alisema kwamba ili Zanzibar iweze kuinuka kiuchumi, lazima mfumo wa muungano ufanyiwe marekebisho, lakini hata hivyo hakufafanua.
Alisema kwamba matatizo ya Zanzibar yanachangiwa na Wazanzibari wenyewe kuwa na kigugumizi katika kufikia maamuzi kwenye masuala mazito yenye masilahi ya nchi.
Alitoa mfano kuwa hivi karibuni Benki ya Dunia imefadhili mradi wa Usimamizi wa Mazingira ya Bahari na Ukanda wa Pwani (MACEMP), lakini Tanzania Bara wameanza kunufaika na mpango huo wakati Zanzibar bado.
Alieleza kwamba Zanzibar imetakiwa kutoa eneo ili kujenga bandari ya uvuvi kwa ufadhili wa mradi huo, lakini hadi sasa viongozi wa SMZ wamekuwa wakivutana juu ya eneo litakalojengwa mradi huo.
Tangu Serikali ya Awamu ya Sita kuingia madarakani na kukubali kuwapo viwango sawa vya kodi baina ya Bara na Zanzibar, wananchi wengi visiwani wamekuwa wakilalamikia kipato chao kuanguka kwa vile soko la ndani limezorota.
Kutokana na hali hiyo, wafanyabiashara wengi waliokuwa wakifuata bidhaa Zanzibar wameacha, na sasa wafanyabiashara wa Zanzibar ndio wanaolazimika kwenda Tanzania Bara kufuata bidhaa, zikiwamo nguo.