CHAMA cha Wananchi (CUF), kimemfungulia kesi ya madai ya sh milioni 500 aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Omari Mahita, kutokana na kukihusisha chama hicho na ujambazi.
Kutokana na kesi hiyo, leo Mahita anapandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu ya Tanzania mbele ya Jaji Laurean Kalegeya.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, CUF pia wanataka walipwe fedha hizo kutokana na Mahita kueleza kuwa waliingiza nchini kontena la visu kwa ajili ya kuvuruga Uchaguzi Mkuu wa rais na wabunge uliofanyika Desemba 14, mwaka jana.
Kesi hiyo namba 72/2006, imefunguliwa na bodi ya wadhamini wa chama hicho, na wanawakilishwa na Kampuni ya uwakili ya Taslima Law Chambers.
Kwa mujibu wa hati hiyo, CUF wanataka kulipwa fedha hizo kutokana na Mahita kuwakashifu kupitia vyombo vya habari, hali iliyowaondolea uaminifu wanachama wa chama hicho.
Inaeleza kuwa Desemba 13 mwaka jana, siku moja kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu, Mahita alitoa taarifa za uongo kuwa wamekamata kontena la visu vilivyoletwa na chama hicho kwa ajili ya kuvuruga uchaguzi.
Hati hiyo inaeleza kuwa Februari 9 mwaka huu, akiwa katika Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, jijini Dar es Salaam, alitamka kuwa chama hicho kinahusika katika wimbi la ujambazi.
“Kutokana na taarifa hizo, vyombo mbalimbali vya habari nchini viliandika taarifa hiyo.
“Siku iliyofuata gazeti la The Guardian ukurasa wa kwanza liliandika ‘CUF has hand in armed robberies’, Majira liliandika ‘CUF wanapanga ujambazi-Mahita’, Tanzania Daima liliandika ‘Mahita: CUF ni majambazi’ na Mwananchi liliandika ‘Mahita atoa mpya. Awahusisha CUF na wimbi la ujambazi’.
Wanaeleza kuwa habari zote hizo ni kashfa dhidi ya chama hicho.
Wanaeleza kuwa kashfa hizo hazina ukweli wowote na kwamba alikuwa na dhamira ya kukichafua chama hicho ili kionekane hakifai katika jamii, hivyo kinapaswa kuepukwa.
Wanaeleza kuwa kutokana na kauli hizo, baadhi ya wanachama walikikimbia chama hicho kwa kuamini maneno ya Mahita.
Hati hiyo inaeleza kuwa licha ya kumwandikia barua ya kumtaka Mahita kuwaomba radhi kutokana na kauli hizo, hakufanya hivyo, licha ya kuthibitisha kuwa barua hiyo aliipokea.
Katika kesi hiyo iliyofunguliwa mahakamani hapo Mei 22, CUF inataka mbali na kulipa fidia hiyo pia alipie gharama za kesi hiyo.
Kesi ya CUF na Mahita imekuja siku chache baada ya mkuu huyo wa zamani wa Jeshi la Polisi kuburuzwa mahakamani katika kesi ya madai ya matunzo ya mtoto inayomkabili.
Mahita anadaiwa kuzaa na aliyekuwa mfanyakazi wake wa ndani, Rehema Shaaban. Rehema ndiye mlalamikaji katika kesi hiyo.
Hata hivyo, Jumanne iliyopita upande wa utetezi wa kesi hiyo, umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kufuta kesi hiyo, kwa maelezo kwamba, imefunguliwa nje ya muda kisheria. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 17 itakapoanza kusikilizwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi, Pellagia Khaday