Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Salehe Mmoro  »  Wenye Vichwa vikubwa na matumbo membamba wapewe keki watunze
Wenye Vichwa vikubwa na matumbo membamba wapewe keki watunze
By Salehe Mmoro | Published  10/20/2006 | Salehe Mmoro | Rating:
Na Mwandishi wa HabariTanzania.com, Dar es Salaam
WENYE VICHWA VIKUBWA NA MATUMBO MEMBAMBA WAMEPEWA KEKI WATUNZE; WENYE VICHWA VIDOGO NA MATUMBO MAKUBWA WAMETUPWA KWENYE KOKOTO!


KATUNI iliyochorwa na King Kinya, katika gazeti, The Citizen la Oktoba 16 mwaka huu, juu ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri aliyofanya Rais Jakaya Kikwete, imeniacha hoi!

Katika katuni hiyo, J.K. amefagia nyumba. Waandishi wa habari, hususan wapiga picha wa Televisheni, wakatimka mbio kwenda kutazama ndani ya pipa la taka; bila shaka wakitarajia waone kilichotupwa humo!

Kwa mshangao, na kinyume cha matarajio,hakuna kilichokuwa kimetupwa humo; hata baada ya harakati za J.K kusafisha hiyo nyumba. “Kwa nini? Hakuna kilichotupwa!”

Mwanzoni mwa mwezi huu, alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari, Rais Jakaya Kikwete alisema, alikuwa akiridhishwa na utendaji wa Baraza lake la Mawaziri. Aliulizwa na waandishi hao, tena wahariri waandamizi wa vyombo vya habari hapa nchini; kama alikuwa akiridhika na utendaji kazi wa Mawaziri!

Wiki mbili tu baada ya kauli hiyo, Rais akabadili Baraza lake. Si hoja Rais kufumua kile alichosuka mwenyewe Januari 4 mwaka huu. Miezi takriban 10 ilikuwa imepita; na chochote kilikwisha fanyika, hata ingawa rais alikuwa akiridhishwa na watu wake.

Kauli za wachambuzi wa masuala ya kisiasa hapa Tanzania ni kwamba, ufumuaji wa Baraza la Mawaziri lililodumu kwa miezi 10 tangu kuzaliwa, ni matokeo ya kushindwa kuendana na kasi ya rais katika kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania. Na baadhi wana hpji: Kwa nini rasis alifagia nyumba, lakini taka hazijaonekana? Ni sayansi ya urejezaji?

Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha na Naibu wake, Lawrence Kego Masha, walitaka kumpaka matope rais: Kutoa ahadi kwamba tatizo kubwa linalohujumu ahadi hii nyeti aliyoahidi rais kwa kila Mtanzania-ya Maisha Bora – la mgao wa umeme, litatoweka punde, baada ya Kampuni ya Kimarekani ya Richmond, kuleta Jenereta ya kuzalisha umeme katika kipindi hiki cha dharura.

Rais alikuwa amewaahidi wananchi, kuwa tatizo la umeme ambao ndio kichocheo kikuu cha uchumi na maisha bora ya watu, lingekuwa la kitambo kidogo! Kinyume chake, ikaja kufahamika kuwa hata huko Marekani kwenyewe, Richmond haijulikani! Ni ‘Mysterious’ Power Company, iliyokwisha zua maswali si Tanzania tu, bali hata Wamarekani wanahoji:

Iko wapi hiyo?

Wamemwaibisha Rais Jakaya Kikwete! Watafanyaje mkataba na kampuni “Hewa”? Wataingiaje mkataba wa aina hii katika suala tete la ukosefu wa umeme? Wizara hiyo ilishindwa kutekeleza majukumu waliyopewa na rais mwenyewe, hata baada ya semina elekezi ya Ngurdoto, iliyofanyika miezi michache tu iliyopita! Walitaka kumkosesha rais uaminifu kwa wapiga kura. Je, watamtii nani?

Ili kulinda heshima yake kwa wananchi waliompigia kura mwaka mmoja tu uliopita, ilikuwa lazima rais afanye kitu…ndio maana waandishi wa habari waliposikia mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, wakatimkia katika “pipa la taka” ili kuona kina nani wamemwagwa humo? Watu walitarajia kungekuwa na “makapi” baada ya rais kupembua ngano na pumba.

Si wizara hiyo moja inayoonekana kukwamisha ahadi ya rais ya maisha bora kwa watu milioni 37

Zipo wizara nyingine ambazo wananchi walikuwa wakisema hazina lolote isipokuwa kujitengenezea ulaji: Wao, watoto wao, nyumba ndogo zao na ndugu na jamaa zao; wakati Watanzania wakihangaika, kwa kukosa nishati iwe ya jua, umeme, mkaa au kuni, na pia huduma na miundo mbinu mbalimbali. Kufuatia mabadiliko haya, baadhi ya wananchi wamesherehekea kwa kuchinja, kuchoma na kumla mbuzi mzima tena baa!

Wengine wamenuna (sijui wamemnunia nani?) baada ya kusikiliza Radio Tanzania ikitangaza mabadiliko hayo Alasiri, Jumapili iliyopita!

Kilichowafanya watu hawa kununa au kufurahi, baadhi ya watu wanadai,ni kama kichwa cha makala hii kinavyosema! Kwamba, “Wenye vichwa vikubwa (Big Mind) na matumbo membamba,ya kufakamia mali ya umma, wenye masikio makubwa ya kusikia kero za wananchi, na wenye macho makubwa ya kuona njia ili kuhimili Kasi Mpya”, wamekabidhiwa ‘keki ya Taifa’ ili wailinde kwa ajili ya Watanzania!

“Wenye vichwa vidogo, vyenye vimacho vidogo, masikio madogo yasiyoweza kusikia kero za wananchi, tena wana vifua vyembamba visivyomudu mwendo kasi wa kuiendea Tanzania yenye neema”, wamepata msituko.

Wana matumbo mapana ya kufakamia kila wakionacho mbele yao !  Wametupwa mahali pakavu, penye kokoto, ili walie na kusaga meno! Binafsi, mimi sipendi kukiamini kichwa cha habari hapo juu, kwa sababu uwaziri ni uwaziri. Uwe wa kukamua maziwa au kuuza njugu, ni uwaziri. Kila Waziri ana heshima zake, ofisi yake na mafao yanayomstahili .

Na uwaziri huo hata uwe wa mitumba, unatokana na kodi za wananchi.

Ninachotaka kusema ni kwamba, waliozomea au kushangilia mawaziri10 na manaibu wanane, kubadilishwa wizara, wanataka kutwambia nini?

Na waliosononeshwa na mabadiliko hayo wanataka tuamini kuwa ndugu zao au jamaa, kama si marafiki zao, walikuwa panono, kabla ya kutupwa penye kokoto? Wanataka tufikiri kuwa huko ‘sehemsehem’ kulikuwa na ulaji? Walikuwa wakituibia, siyo?

Kama si hivyo, kusikitika kwa nini? Kusononeka kwa kazi gani? Na shangilizi zatoka wapi? Kuzomea kwa mpango upi?

Watanzania wange tahayari. Kama mwenye nyumba (rais Kikwete) kafagia nyumba, na taka hazijaonekana, baada ya kuzirejeza (recycled) tunapaswa kujiuliza: Huko walikopelekwa watafaa?

Wataweza kasi? Watabadili tabia ili wawatumikie wananchi, badala ya kutumikia matumbo yao ?

Nathubutu kusema ‘matumbo’ kwa kuwa wapambe wa baadhi yao walionekana wakipigiana simu kupeana ‘pole’ kwa sababu ya mabadiliko hayo! Narudia: Pole ya nini? Sononeko, huzuni, simanzi na kunyong’onyea kunakujaje, kama si hofu dhidi ya matumbo yao na vichwa vidogo?

Wapo mawaziri wengine waliobadilishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine si kwa sababu ya kuboronga, huko walikotoka. Tunadhani taaluma zao na ‘Vichwa vikubwa’ walivyo navyo katika nyanja walizopewa kuongoza, vitatusaidia kufanyiwa majaribio ya unyozi na kila ajaye.

Watanzania wamechoshwa na maneno matupu na majaribio ya sera. Wanataka mikakati itakayowaondolea ukosefu wa maji, umeme, umasikini, magonjwa,ujinga, unyang’au na kila vizingiti katika barabara ya maendeleo.

Katika dhiki tuliyo nayo ya ukosefu wa nishati, kwa nini serikali kuingia mkataba na kampuni ‘hewa’ badala ya kufanya kweli, ili tuwe na umeme wa uhakika? Kwa nini kujiingiza kichwakichwa kwa matapeli? Vichwa vidogo; matumbo makubwa? Kama nilivyokwisha sema sipendi kuamini hivyo.

Wengine wanasema wapo mawaziri waliokwisha choka! Wamwechoshwa na nini? Wanabeba kokoto? Wanabeba matumbo? Wachoshwa na nini! Wamepewa nguvu, ari na kasi mpya. Wamechokaje asilimia tano tu ya mwendo wa miaka mitano? Kwa nini wasijiuzulu tangu Ngurdoto?

Hapa, bila shaka kuna ukweli unafichika. Ndio maana wengi walikimbilia kuangalia kina nani wataachwa, ili wazue tetesi, wakakuta ndani ya pipa la taka, hakuna taka. Tunatakiwa kuamini kuwa, rais Kikwete amewapa muda mawaziri wake kufanya kazi kwa kutumia vichwa vikubwa (Big mind) na wala si matumbo makubwa.

Tunasubiri ubunifu es kisayansi. Ataumechoshwa na hadithi za baadhi ya mabwanyenye kutumia dhiki zetu kujineemesha. Madaraja mabovu, ndege mbovu, mabarabara mabovu, mikataba hewa, jenereta hewa n.k Kwa mara nyingine Watanzania hawataki kutilia mashaka utendaji kazi wa Baraza la Mawaziri la rais Jakaya Kikwete. Tunataka kupokea ahadi zinazotekelezwa toka kwa viongozi wetu.

Tunamshauri rais Kikwete aache ‘huruma’ kwa mawaziri wenye vichwa vya mbuzi, lakini wenye matumbo ya ngamia. Hawaifai Tanzania . Wa nini? Sehemu yao ni katika pipa la taka lililotupu nje ya ikulu.

Wanachelewesha maendeleo…maneno matupu, lakini hakuna kinachoonekana. Hawana masikio, hawana macho, ila madomo mapana na matumbo ya kuifukarisha jamii kwa uroho wao. Kama sivyo kwa nini mipango hewa? Kwa nini usanii kwenye msiba kama wa kukosa umeme, maji, barabara, mkaa, na umasikini vijijini?

Mwisho, napenda kumpongeza rai Kikwete. Wiki mbili zilizopita, alikuwa akiridhishwa na utendaji kazi wa Baraza lake la Mawaziri. Lakini, mara baada ya mashaka, pengine yaliyotokana na maswali ya waandishi wa habari, akafanya mabadiliko.

Tunamuunga mkono kwa dhati, ila tunaomba akaze fagio lake; chini ta zulia analokanyaga, kuna vumbi, uchafu, dumuzi na mende wanaojificha, ili kusubiri giza wabungue ‘keki ya Taifa’. Wametikiswa, hawajatikisika! Shime wapukutishwe na kutupwa, ili liwe fundisho kwa wenzao. Hakuna kungoja.

Wale ambao wapambe wao wanasononeshwa au kufurahi kwa sababu ya wizara mpya walizopangiwa, wamulikwe kwa kurunzi kali. Si bure; kuna kitu…

Wapo wanaosema rais katupiga chenga ya mwili. Walitarajia hatua kali dhidi ya mawaziri walioshindwa kufanya kitu. Walitarajia kuwaona jaani. Wamepewa nafasi ya pili. Ama ukivaa kiatu cha kushoto, ukagundua kosa lako, utakitupa au utatazama wapi ulikosea? Sasa rais karekebisha viatu miguuni pake, twatazamia kasi halisi.

Kama hili halitawezekana, tunajiandaa kushindwa baada ya kushindwa kujiandaa?

omybabu@yahoo.com


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by sitojo)
    Rating
    Ni kweli mzee kauli mbiu hazitatufikisha mahali popote. rais hawezi kufanyakazi peke yake na kila mtu akimwangalia yeye aweze kutufikisha tunakokwenda. Tunapaswa kumsaidai. Kuna vyombo vya kitaifa ambavyo vina kazi hiyo, bunge, mahakama. Ikiwa hivi vyote vitadhibitiwa na serikali ya chama tawala, basi tujui tutabidi kukodoa macho kumwangalia mwokozi rais. Kama nae anasema funika kombe mwanaharamu apite tumeumia.
    Chama kimoja kinaweza kujenga uchumi sikatai, mifano ipo. China, Urusi, lakini wenzetu wanamalengo. Bila kuwa na malengo sahihi hatufatika. Na mshika mbili moja humponyoka. Tunataka nini kwanza ambacho ndio chachu ya maendeleo. Jibu nishati. Tushughulikie nishati kama hatua akili nzuri hadi tuwe nayo. Pili miundo mbinu, barabara , mawasiliano ya simu na kadhalika. Tushughulikie kama vile hakuna kingine cha kushughulikiwa. Tukikamilisha hayo mnaweza kutawala mnavyotaka . Kila kitu kitajileta wenyewe. Wawekezaji watakuja kama hawana akili nzuri vile. Lakini namna hii tutashindwa kufika popote. Ni karibu mwaka sasa tangu JK achaguliwe kuwa rais na hadi sasa hakuna umeme.maendeleo yaliyokwisha patikana si yanarudi nyuma. najisikia vibaya hata kusema mwaka huu nije nyumbani Tanzania, Nasubiri umeme.
    Ahsante.
     
Submit Comment


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Is Tanzania a safe place to invest?
  4. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Linda Garner
  4. Nthelezi Nesaa
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.