Rais Jakaya Kikwete ametia ngumu Tanzania kupeleka majeshi yake kulinda amani huko Darful nchini Sudan iwapo suala la kugharamia vikosi hivyo halitatafutiwa ufumbuzi.
Amesema Tanzania haiko tayari kuingizwa mkenge tena na kubebeshwa gharama kibao kama ilivyotokea huko Liberia miaka iliyopita.
Amesema Tanzania itakuwa tayari tu kupeleka majeshi yake iwapo suala la gharama za majeshi hayo na vifaa vya kivita litatafutiwa ufumbuzi kwanza.
Alisema taifa haliko tayari kabisa kugharamia majeshi yake yakiwa huko Darful kwa ahadi ya kurejeshewa gharama zake.
Amesema sababu kuu ya kukataa kutuma majeshi nchini humo ni kuliepushia taifa mzigo mkubwa wa gharama, wakati lenyewe lina matatizo kibao na majukumu makubwa ya kukwamua maisha wa raia wake.
Rais Kikwete amesema Tanzania imejifunza kutokana na ’mkenge’ ilioingizwa miaka ya 1990 ilipotuma vikosi vyake katika nchi ya Liberia na kujikuta ikiingia gharama kubwa.
Amesema walipopeleka wanajeshi wao walitumaini mzigo wa gharama ungebebwa na Umoja wa Mataifa lakini badala yake Serikali ikagharamika kuwarejesha na kuwalipa askari hao, kitu ambacho hataki kitokee tena.
Rais aliyerejea nchini juzi akitokea nchi za Ulaya na Asia, amesema kuwa kutokana na tukio hilo la Liberia, katu hatakubali nchi kuiingizwa tena mkenge kwa kupeleka vikosi vyake eneo hilo la Darfur lililojaa machafuko.
Alisema pia Tanzania haiko tayari kupeleka vifaru vyake na vifaa vya kijeshi huko.
hata hivyo amesema iwapo gharama na vifaa vya kijeshi vitatolewa, yeye hana hiana atatuma vijana wa kazi kulinda amani.
Rais amesema hayo katika mahojiano yake maalum na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC),Idhaa ya Kiswahili yaliyosikika mapema leo asubuhi.
Katika mahojiano hayo pia Rais Kikwete ameelezea mafanikio ya ziara yake na jinsi alivyopokelewa na kueleweka kwa viongozi wa nchi wahisani walioahidi kuisaidia Tanzania.
’Kwa kweli nchi wahisani wamenipokea na kunipongeza kwa mwenendo wa nchi yetu na kuahidi kutusaidia kwa hali na mali, hii ni faraja kwangu na kwa taifa kwa ujumla,’ Rais akasema.