KAMPUNI ya simu za mkononi ya Celtel, imekabidhi hundi zenye thamani ya sh milioni 57 kwa washindi 21 wa promosheni ya ‘Jishindie ndoto yako’.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kukabidhi hundi hizo jana katika Hoteli ya Holiday Inn, Meneja Masoko wa kampuni hiyo, Margaret Kositany alisema miongoni wa washindi hao, wanne ni wa hundi ya milioni 10 kwa kila mmoja na washindi 17 ni hundi ya sh milioni moja kila mmoja.
Alisema lengo la Celtel ni kuboresha maisha ya wateja wanaoendelea kupata huduma za mawasiliano na kuwapa fursa zaidi za kuboresha maisha yao.
“Lengo letu Celtel ni kuhakikisha kuwa tunaboresha maisha ya wateja wetu na tunafanya juu chini kuhakikisha kuwa wanaendelea kupata huduma bora za mawasiliano, pia kuwapa fursa za ziada za kuboresha zaidi maisha yao,” alisema Margaret.
Akizungumza baada ya kupokea hundi ya sh milioni 10, Selemani Mohamed Shemndoro (46) ambaye ni mkazi wa Majumba Sita, Ukonga, Dar es Salaam, aliishukuru kampuni hiyo na kuahidi kutumia fedha hizo katika kuendeleza biashara zake na familia.
Washindi wengine wa sh milioni 10 ni Mussa Mbwilo, Yusuf Rajabu na Zahara Abdu.