VYUO vya ualimu nchini, vimeshauriwa kutoa walimu wenye uwezo wa kufundisha stadi za kazi katika shule za msingi nchini.
Ushauri huo umetolewa jana na Mjumbe Mwangalizi wa Elimu, Mwajuma Nyiruka kwenye warsha ya viongozi mbalimbali kutoka katika taasisi ya elimu na walimu wa shule za msingi kutoka katika mikoa mbalimbali nchini waliokuwa wakijadili kuboresha ufundishaji wa stadi za kazi kwa wanafunzi wa shule za msingi ambao umedorora kwa muda mrefu bila mafanikio
Alisema wakiwapo walimu wa aina hiyo, watasaidia shule kuzalisha mali yenyewe kupitia somo hilo.
Naye mjumbe wa Oxfam GB Tanzania, James Sangoro, aliwashauri walimu kufundisha somo hilo kwa kutumia mifano hai ya vitu vinavyozunguka na kuwashirikisha wanajamii wenye ujuzi na utaalamu wa kutengeneza mambo mbalimbali kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi somo hilo kwa vitendo.
Alisema hivi sasa somo hilo halifundishwi kwenye baadhi ya shule kutokana na ukosefu wa vifaa vya kufundishia, walimu kutokuwa na ufahamu wa kutosha kufundisha somo hilo, kutokuwapo kwa semina elekezi kwa somo husika kwa walimu, na uhaba wa walimu wa stadi za kazi.
Alisema matarajio ni kupata mwongozo mpya kwa nchi nzima kuhusu ufundishaji wa somo hilo, kusikia maoni ya serikali na asasi zsizo za kiserikali kuhusu matatizo ya ufundishaji wa somo, kupata ujuzi, maarifa na mbinu za stadi za kazi na kujua utaratibu utakaotumika kutahini somo hilo