WAZIRI wa Maji, Dk. Shukuru Kawambwa, amewataka wafanyakazi wa wizara hiyo kuwa wabunifu na wachapakazi, ili kuweza kufanikisha malengo ya wizara kwa wakati.
Alisema hayo jana alipokuwa akijitambulisha kwa wafanyakazi wa wizara hiyo baada ya kuteuliwa hivi karibuni kuongoza wizara hiyo.
Alisema wizara hiyo ni tegemeo kubwa la wananchi wa kada zote, hivyo ni lazima washirikiane kwa pamoja katika kufanya kazi na kufikia malengo.
“Binafsi nawahakikishia nitawapa ushirikiano wa kutosha na nyie naombeni ushirikiano wenu wa hali na mali kwa kuwa nyie ni wazoefu katika wizara hii. Milango iko wazi, ninaomba watendaji wangu tuchape kazi.
“Nitaava viatu vile vile vya aliyekuwa Waziri wa wizara hii, Steven Wassira kwa maana nitaendeleza mazuri aliyokwishayaanza, lengo likiwa ni kusonga mbele na kuhakikisha watu wanapata maji,” alisema Dk. Kawambwa.
Wakati huohuo, wafanyakazi hao walimweleza Waziri Kawambwa kuwa Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS) wizarani hapo kimejaa ubabaishaji kwa kuwa kimekuwa kikikopesha watu ambao si walengwa, hivyo kumwomba aubadilishe uongozi wa chama hicho.
Walisema wamekuwa wakikopeshwa magari mabovu wakati uongozi wa SACCOS hiyo kabla ya kuwakopesha unawaambia kuwa ni magari mapya kutoka nchini Japan.
Hata hivyo, Waziri Kawambwa aliwaahidi kushughulikia tatizo hilo na kusema kuwa atakaa na menejiment kuona watalitatua vipi tatizo hilo.