UAMUZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hususan wa Kamati Kuu ya chama hicho, kulipitisha jina la Amaan Kabourou kuwa miongoni mwa wagombea ubunge wa Afrika Mashariki, umeshaanza kuzua maneno ya chini chini na wasiwasi miongoni mwa wagombea wengine wa nafasi hiyo.
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kwamba, hatua ya chama hicho tayari imeibua hisia zinazokinzana, ambazo zinaweza zikawa na athari katika mwenendo mzima wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu.
Baadhi ya wagombea ubunge wa Afrika Mashariki kwa tiketi ya chama hicho waliozungumza na gazeti hili, kwa sharti la kutoandikwa majina gazetini walisema, hali imekuwa ni ya kukatisha tamaa kutokana na ukweli kwamba, Kabourou anaonekana kuchukua sura ya kuwa mgombea wa chama.
Mgombea mmoja ambaye ni kada wa muda mrefu wa chama hicho tawala alisema, tangu ajiunge na CCM hivi karibuni, Kabourou ametokea kuwa kipenzi kikubwa cha Katibu Mkuu wa chama hicho, Yussuf Makamba na hivyo kuchukua sura inayoonyesha kuwa anaungwa mkono na chama kwa ujumla.
“Sisi wagombea wanaume kutoka Tanzania Bara tuna nafasi tatu za ubunge huo. Hata hivyo hali inaonyesha kuwa ngumu, kwa sababu ya chama na hususan Makamba kuonekana dhahiri akimbeba Kabourou,” alisema mgombea mmoja wa ubunge huo.
Mgombea mwingine alilieleza gazeti hili kwamba, ingawa lengo la Makamba na CCM ni kulenga kuudhoofisha upinzani kwa kumpigia debe Kabourou, hatua hiyo kwa upande mwingine inawapunguzia imani makada wa muda mrefu, ambao wanajiona kuwa wamekuwa ni waaminifu wakubwa kwa chama chao.
“Hali hiyo kwa kweli itasababisha kura zipigwe kwa mwelekeo huo, kwani wabunge wa CCM watajikuta wakilazimika kumpigia Kabourou kwa sababu tu ya kuonekana kwake akiwa ndiye mgombea wa chama, hali ambayo kimsingi si nzuri,” alisema mgombea mwingine wa ubunge aliyezungumza na Tanzania Daima.
Wagombea hao wanasema, tayari hali ndani ya chama hicho imeanza kuonyesha kwamba, Makamba amekuwa akiongoza kundi la viongozi wanaolalamikiwa kwa kuwabeba “wageni” ndani ya chama hicho.
“Wapo wagombea wenzetu wanaotamba wazi wazi kuwa wana baraka za Katibu Mkuu.
“Hili si jambo la kificho tena, wanatamba wakisema wana uhakika wa kupita. Mambo haya yanatuumiza sana sisi ambao tumekuwa waaminifu kwa chama chetu kwa miaka yote,” alisema mmoja wa wagombea hao.
Katika malalamiko hayo, mwanachama mwingine mgombea alisema mchujo uliofanywa, ingawa yeye amefanikiwa kupita, lakini hakufurahiwa na baadhi ya wagombea ambao anajua walikuwa wapinzani mahiri wa sera na itikadi za CCM.
“Hawa wamewezaje kuwa malaika ghafla? Watu waliosimama kuitukana CCM, leo wanarejea, wanakaribishwa na kupewa heshima kubwa ya kuwania uongozi nyeti katika taifa letu,” amesema.
Miongoni mwa wanaosemwa ni aliyekuwa mwanachama na kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na Mbunge wa Kigoma Mjini, Dk. Kabourou.
Dk. Kabourou, pamoja na Hiza Tambwe, aliyekuwa mmoja wa viongozi waandamizi wa Chama cha Wananchi (CUF), mwezi uliopita walirejea CCM na kupokewa kwa mbwembwe.
Tangu arejee CCM, Tambwe amewapiku wanachama wengine wa chama hicho kwa kuwa karibu zaidi na Makamba.
“Tangu arejee, amekuwa karibu na Makamba, kiasi kwamba kila mahali anaonekana. Waliokuwa wapambe wanalalamika.
“Hili linaonekana sasa kuwa jambo la kawaida kwani kabla ya kuwapo Makamba, Mangula (Philip) naye alizungukwa na watu kama kina Msabah waliotoka CUF,” amesema mgombea mwingine.
Malalamiko ya wanachama hao yanajikita katika mwenendo mzima, wakianzia kwenye nafasi mbalimbali, zikiwamo za ubunge.
Wanatoa mfano kwamba Danhi Makanga, kabla ya kujitoa United Democratic Party (UDP) na kurejea CCM, alikuwa akikosoa wazi wazi sera za CCM na kuonyesha kasoro nyingi za wazi.
Kasoro hizo zingalipo, lakini tangu arejee CCM, ameweza kuwa mtetezi mahiri wa yote aliyoyakuta.
Muda mfupi baada ya kujitoa UDP, alijiunga CCM na kuwania ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Bariadi Mashariki. Alimshinda kwa mbinde mgombea wa UDP na Mwenyekiti wa chama hicho, John Cheyo.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Cheyo alilipiza kisasi cha kisiasa kwa kumshinda Makanga.
Kwa kuendeleza utaratibu wa kuwakumbatia waliokuwa wapinzani wa CCM, Rais Kikwete, naye akaendeleza ya waliomtangulia. Akamteua Makanga kuwa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Kwimba mkoani Mwanza.
Hali kama hiyo ilikuwa kwa mwanachama mwingine wa UDP, Teddy Kasela-Bantu. Teddy, baada ya kujitoa katika chama hicho, alijiunga CCM, na haraka haraka akapewa heshima ya kukiwakilisha chama hicho kwenye kinyang’anyiro cha ubunge. Kwa sasa ni mbunge wa Bukene.
Hali kama hiyo ilishajitokeza kwa Dk. Masumbuko Lamwai, ambaye baada ya kukikimbia chama chake cha NCCR-Mageuzi, alikaribishwa CCM.
Bila kuchelewa, aliyekuwa rais kwa wakati huo, na Mwenyekiti wa CCM, Benjamin Mkapa, akamteua kuwa mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Pia alipewa nafasi muhimu ndani ya chama hicho.
Aliyekuwa Mbunge wa Njombe Magharibi, Thomas Nyimbo, kabla ya kujiunga CCM, alikuwa mwanachama mwaminifu wa chama cha siasa cha PONA.
Akiwa katika chama hicho, aliichachafya CCM, kiasi cha kuifanya ianze mipango ya kumnasa; jambo ambalo baadaye lilikuwa la kweli.
Alipokewa CCM na kupewa baraka zote za kuwania ubunge. Alifanikiwa kushinda, kabla ya kutupwa nje kwenye kura za maoni mwaka jana.
Katika Baraza la Mawaziri la sasa, wamo waliokuwa wanachama wa vyama vya upinzani. Miongoni mwao ni Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Stephen Wasira na Naibu Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni, David Nsanzungwanko.
Tofauti na wapinzani wengine, Wasira aliihama CCM kutokana na kutotendewa haki, na kufanyiwa mizengwe licha ya kuibuka mshindi kwenye kura za maoni.
Kitendo cha viongozi wa juu wa CCM kuwakumbatia “wahamiaji”, kinawaudhi wanachama wengi ambao wanadhani kwa uadilifu na mapenzi yao kwa chama chao, wangekuwa wa kwanza kufikiriwa pindi unapowadia wakati wa uchaguzi.
Wiki hii, Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM iliyokutana chini ya Mwenyekiti wake, Rais Kikwete, ilipitisha majina 38 ya wanachama watakaowania ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Waliopitishwa kwa upande wa Tanzania Bara ni George Nangale, Dk. Norman Siggala, Samwel Wangwe, Dk. Didas Masaburi, na Dk. Michael Ndanshau.
Wengine ni Dk. Kabourou, Dk. Baanda Salim, Evod Mmanda, Dk. Handley Mafwenga, Renatus Mkinga, Goodluck ole-Madeye na Mwabani Kambangwa.
Wagombea wengine ni Anamringi Macha, Dk. Richard Kassungu, Joseph Kessy, Rogers Shemwelekwa, Gideon Mandes, Eliachim Simpasa, na Aloys Mwasongwe.
Kwa upande wa wanawake ni Kate Kamba, Hulda Kibacha, Dk. Terezya Huvisa, Janet Mmari, Rose Maeda, Janet Mbene, Neema Nshumba, Hadija Kusaga na Eva Makune.
Wagombea kutoka Zanzibar ni Balozi Isaack Sepetu, Nassoro Juma Mugheir, Dk. Said Gharib Bilal, Abdallah Ali Hassan Mwinyi, Remedius Edington Kissassi, Dk. Yusuf Nuhu Pandu, Dk. Makame Ali Ussi na Rajabu Uweje Yakubu.
Kwa upande wa Zanzibar wagombea wanawake ni wawili; Mahfoudha Alley Hamid na Sebtuu Mohamed Nassoro.
Oktoba 29, mwaka huu utafanyika mchujo wa mwisho kabla ya majina kupelekwa mbele ya wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kupigiwa kura.
Tanzania, Kenya na Uganda; kila moja inatakiwa itoe wabunge tisa. Kwa hapa nchini, uwakilishi huo unazingatia pande mbili za Muungano, jinsi, na uwiano kati ya chama tawala na vyama vya upinzani. Upinzani una kiti kimoja pekee.
Habari zinaeleza kwamba, tayari jina la Rais Jakaya Kikwete limeshaanza kutumiwa na baadhi ya wagombea kama chambo cha kupata kura