Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein, amesema kuwa Serikali itahakikisha kwamba hakuna mtu atakayekufa njaa kwenye maeneo yote yaliyokumbwa na mafuriko mkoani Kilimanjaro.
’’Serikali itahakikisha kwamba inatoa kila aina ya msaada kwa wote waliopatwa na janga la mafuriko na kuwasaidia kurejea katika maisha yao ya kawaida,’’ alisema Dk. Shein.
Aliyasema hayo katika mkutano wa hadhara alipozungumza na wakazi wa kijiji cha Mandaka Mnono kitongoji cha Uswahilini, moja ya maeneo yaliyokumbwa na mafuriko.
Mafuriko hayo yalivikumba vijiji 16 vya Moshi ambavyo vipo katika kata nne za Kahe, Old Moshi Magharibi, Kirua Vunjo Kusini na Kahe Mashariki.
Katika ziara hiyo ambayo ilikuwa na lengo la kuwapa pole wananchi walioathirika, Dk. Shein alifuatana na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge) Bw. Juma Akukweti.
Katika ziara hiyo, Dk. Shein alizunguka kwa helikopta ili kujionea athari ya mafuriko hayo na aliwaambia wananchi hao kuwa amejionea athari hiyo na akawahakikishia kwamba hakuna atakayekufa njaa.
’’Serikali italeta chakula na kitagawiwa bure kwa walioathirika na kwa wale walioharibikiwa nyumba zao jitihada za kuwahifadhi zinafanywa,’’ alisema.
Kwa upande wao wananchi walimwomba Makamu wa Rais kuwajengea shule na zahanati kwa kuwa huduma hiyo hawana hivyo kulazimika kufuata huduma hiyo eneo la mbali.