MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala, imemtaka Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, John Lubuva, kutoa sababu za kukiuka amri ya mahakama na kuwafukuza wafanyabiashara ndogo ndogo au wamachinga kwenye maeneo yao ya biashara isivyo halali.
Amri ya kuitwa mahakamani mkurugenzi huyo, ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Bahati Ndesaruwa, alipokuwa akisikiliza maombi ya wanachama wa jamii ya maendeleo ya kutaka mkurugenzi huyo kufungwa jela au kupewa adhabu kali kwa kukiuka amri ya mahakama na kuwabughudhi wamachinga hao.
Awali, wakili wa mkurugenzi huyo, Mponela, aliiomba mahakama kumpa muda ili mteja wake awasilishe majibu ya hati ya kiapo cha walalamikaji iliyowasilishwa mahakamani hapo Oktoba 2, mwaka huu na wakili wao, Aboubakar Salim wa Kampuni ya uwakili ya Taslima.
Baada ya maombi ya wakili Mponela, upande wa walalamikaji uliomba mahakama kutoa ruhusa ya wamachinga hao kuendelea na biashara zao kwenye maeneo ya awali wakati mahakama inasubiri majibu ya mkurugenzi.
Kabla ya kuahirisha shauri hilo hadi Oktoba 26, mwaka huu litakapotajwa tena, Hakimu Ndesaruwa, alisema mahakama itasubiri kwanza sababu za mkurugenzi kabla ya kuamua ama kuwaruhusu wamachinga au kuendelea na shauri hilo.
Dai la msingi la wamachinga hao ni kutaka kurejeshwa katika maeneo hayo na kutambuliwa kihalali. Pili, wanataka walipwe sh milioni 2.5 kila mmoja kama kifuta jasho kwa ajili ya usumbufu walioupata kutoka kwa mkurugenzi na wafanyakazi wa manispaa ya Ilala.