UPANDE wa utetezi katika kesi ya madai ya matunzo ya mtoto inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Omari Mahita, umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kufuta kesi hiyo kwa maelezo kuwa imefunguliwa nje ya muda kisheria.
Pingamizi hilo liliwasilishwa jana mahakamani hapo na wakili wa utetezi, Charles Semgalawe mbele ya Hakimu Mkazi, Said Msuya wakati kesi hiyo iliyohudhuriwa na umati wa watu ilipotajwa kwa mara ya pili.
Wakili huyo alisema kuwa, mlalamikaji amechelewa kufungua madai hayo.
“Kisheria, alitakiwa kuwasilisha madai hayo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja baada ya kujifungua na kuona kuwa hapati matunzo ya mtoto huyo,” ilieleza sehemu ya pingamizi hilo. Pia alisema mahakama hiyo (ya Kisutu) haina uwezo kisheria wa kusikiliza kesi za aina hiyo.
Katika pingamizi hilo, wakili wa Mahita alisema madai ya aina hiyo husikilizwa na mahakama za chini na si za mkoa kama mlalamikaji, Rehema Shabani, alivyofanya.
Pia mlalamikaji huyo alikiri kupokea maelezo ya utetezi kutoka kwa wakili wa mlalamikiwa. Baada ya kupokea pingamizi hilo, hakimu Msuya, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 17 itakapoanza kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Pellagia Khaday, ambaye jana hakuwapo.
Madai ya msingi ya mlalamikaji huyo ni kutaka kulipwa sh 100,000 kila mwezi na Mahita, kuanzia mwaka 1997 alipojifungua mtoto Juma, hadi atakapomaliza shule. Kwa sasa mtoto huyo anasoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi Muungano, katika Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Katika utetezi wa Mahita, alikiri kumpeleka mtoto huyo nyumbani kwa Sheikh Yahaya Hussein kwa ajili ya kujifunza Quran baada ya mlalamikaji kumtelekeza nyumbani kwa dada wa mlalamikiwa.
Hati ya utetezi ya mlalamikiwa, ilimkana mtoto huyo kwamba si wake na kumtambua mlalamikaji kama mtumishi wake wa ndani kwa kipindi cha mwaka 1995 na si 1996 kama anavyodai mlalamikaji