Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Harufu ya damu yalichafua taifa
Harufu ya damu yalichafua taifa
By Habari Tanzania | Published  10/18/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Waandishi Wetu

MATUKIO ya vurugu na mapambano ya ana kwa ana yaliyosababisha umwagaji damu kwa maana ya mauti na majeruhi, yameendelea kuliandama taifa katika mikoa miwili ya Dar es Salaam na Kilimanjaro.

Moja ya matukio hayo, ambalo limesababisha kifo cha mtu mmoja na mwingine kujeruhiwa kwa risasi, limetokea juzi usiku Mbagala, jijini Dar es Salaam, likimlenga mhasibu wa Wizara ya Miundombinu.

Tukio hilo linaloashiria mazingira ya mauaji ya kukusudia yenye lengo mahususi, limesababisha kuwapo kwa hali ya wasiwasi mkubwa katika wizara hiyo ambayo hadi majuzi ilikuwa ikiongozwa na Waziri Basil Mramba.

Mbali na tukio hilo, kwa mara nyingine tena, Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), jana walilazimika kutuliza vurumai kubwa iliyoanzishwa na wamachinga katika eneo la Mchikichini, Dar es Salaam, zilizosababisha majeruhi kadhaa.

Tukio la Mchikichini ambalo ni mwendelezo wa matukio ya mapambano kati ya wamachinga na askari wa manispaa lilisababisha hali ya wasiwasi mkubwa katika eneo hilo ambalo ni moja ya maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya wafanyabiashara hao.

Huko Rombo, mkoani Kilimanjaro, makandarasi wa Kichina wanaojenga barabara, walijikuta katika vuta nikuvute na polisi, hali ambayo hatimaye ilisababisha askari kupigwa na kujeruhiwa.

Taarifa kutoka huko zinaeleza kwamba, Wachina hao walifanya kitendo hicho baada ya kuvamia kituo kidogo cha polisi kilichopo Tarakea na kuanza kuendesha kipigo kwa kila waliyemkuta kituoni hapo.

Habari za awali zinaeleza kwamba, Wachina hao wakiwa na mapanga mikononi, walivamia kituo hicho, wakati walipokuwa wakijaribu kumwadhibu dereva mmoja wa lori la ujenzi na kukimbilia kituoni hapo kukwepa kipigo ambacho alikuwa amekipata kutoka kwa makandarasi hao wa kigeni.

Tukianza na tukio la jijini Dar es Salaam, mchuuzi wa juisi, jana alinusurika kupoteza maisha baada ya kupata kipigo kutoka kwa mgambo wa Manispaa ya Ilala, wakati wa operesheni ya kuwaondoa wachuuzi wa biashara ndogo ndogo ambao walikuwa wamepanga bidhaa zao pembezoni mwa barabara ya Uhuru eneo la Kituo cha mabasi cha jirani na Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Mkasa huo ulimkuta mchuuzi huyo ambaye hakuwa na hili wala lile, ambaye alikuwa akikokota toroli lake kuelekea eneo hilo na ghafla kuona wenzake wakitimuliwa na mgambo hao.

Mchuuzi huyo ambaye alishuhudiwa na Tanzania Daima, alitimua mbio kurudi alipotoka eneo la jirani na Uwanja wa Karume na aliangukia mikononi mwa mgambo ambao walimpa kipigo na kumuacha chini bila msaada baada ya kumtelekeza.

Hali hiyo iliwafanya wachuuzi wenzake kumbeba na kumpeleka kivulini huku wakipaza kelele wakiwaambia mgambo hao kuwa wameua. “Mmeua, mchukueni mtu wenu mumpeleke kwa Kikwete akaone mambo mnayofanya,” alisema mchuuzi mmojawapo.

“Sijui hii serikali ina agenda gain, kwani hivi sasa nchi hii imekuwa ya timu ya taifa, waandishi wa habari na wafanyakazi wa maofisini, hawatutaki kabisa wamachinga,” alilalama mmoja wao.

Sakata hilo, lilianza mapema alfajiri wakati wachuuzi hao walipofika eneo hilo kama kawaida kwa ajili ya kuanza biashara zao na kukuta vibanda vyao vilivyojengwa mbele ya soko la Mchikichini vikiwa vimebomolewa huku kukiwa na doria ya askari polisi wenye silaha pamoja na mgambo wa jiji.

Wachuuzi hao wakiwa katika makundi, waliamua kuwavurumushia mawe askari hao hali iliyozua hekaheka kubwa na kusababisha kuitwa kwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ambao walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.

Akizungumza na Tanzania Daima, Mwenyekiti wa soko hilo, Jobu Mwakatobe, alisema anashukuru kuondolewa kwa vibanda hivyo kwani walikuwa hawaishi kwa amani kutokana na wamachinga hao kupigana mapanga mara kwa mara kutokana na kugombania maeneo, licha ya kujua kisheria kuwa eneo hilo halitakiwi kufanyia biashara.

Mbali na kukatana mapanga, pia alisema kuwa walikuwa wamejiandaa na matairi ambayo walipanga kuyatumia kuchoma soko zima endapo serikali ingepanga kuwaondoa eneo hilo.

“Kwa upande wangu, kwa kweli najisikia amani kuondolewa kwa watu hawa kwani walikuwa wanatunyima hata usingizi kutokana na vitisho vyao vya kutaka kuchoma soko japokuwa tulikuwa tukijitahidi kufanya nao vikao, lakini pia haikusaidia,” alisema.

Katika tukio jingine baya, Mhasibu wa Idara ya Utawala katika Wizara ya Miundombinu, Joachim Ndibalema usiku wa kuamkia jana, alijikuta akijeruhiwa kwa kupigwa risasi na watu ambao malengo yao hayakuweza kubainika mara moja.

Mbali ya kumjeruhi mhasibu huyo, wahalifu hao walimuua kwa kumpiga risasi, Rwechingura Ndibalema ambaye ni mdogo wa mhasibu huyo. Tukio hilo lilitokea juzi usiku, nyumbani kwa mhasibu huyo, Mbagala Kichemchem.

Mmoja wa wafanyakazi wa wizara hiyo, aliiambia Tanzania Daima kuwa wahalifu hao walivamia nyumbani kwa mhasibu huyo saa 2.00 usiku wakati Ndibalema akiwa sebuleni akijipumzisha na familia yake.

Inadaiwa kuwa, kabla ya kuingia sebuleni, walimjeruhi mlinzi wa nyumba hiyo na kumwamuru awaonyeshe alikokuwa mhasibu huyo, na alikubali kuwasindikiza hadi sebuleni alipokuwa amekaa akiangalia televisheni.

“Waliingia ndani ghafla na kumpiga mvulana wa kazi na kumjeruhi, wakimuamuru aonyeshe chumba ambacho familia yangu ilikuwa imekaa,” alisema mhasibu huyo alipohojiwa na Tanzania Daima akiwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

“Walimpiga mdogo wangu kwa risasi kisha wakanirudia mimi na kunipiga kwa risasi, zilipowaishia walichukua mapanga na kuendelea kunipiga mimi,” alisema.

Mhasibu huyo ametolewa risasi ubavuni na mfanyakazi wake amelazwa katika hospitali hiyo hiyo, wote wakiwa na hali mbaya.

Katika hali ya kushangaza, wahalifu hao hawakuchukua kitu chochote katika nyumba hiyo kwani waliondoka baada ya kumaliza kazi hiyo wakidhani walikuwa wamewaua wote wawili, yeye na mdogo wake.

Habari zaidi ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka Wizara ya Miundombinu alikokuwa akifanya kazi mhasibu huyo zinaeleza kwamba, upo uwezekano mkubwa kuwa tukio hilo linahusishwa na mipango ya kundi fulani la watu au mtu kujaribu kumuua mhasibu huyo kama njia ya kupoteza ushahidi wa ubadhirifu mkubwa wa fedha uliopo katika sehemu zilizo chini ya Ndibalemba kiuangalizi.

Ofisa mmoja wa juu wa wizara hiyo aliyezungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutotajwa jina gazetini alisema, kumekuwa na wasiwasi wa namna hiyo wizarani hapo, hasa kwa kuzingatia kuwa mhasibu huyo ndiye ambaye amekuwa akihusika na masuala ya fedha kwa viongozi takriban wote wakuu wizarani hapo.

“Kwa namna hali ilivyo pale wizarani hivi sasa kuhusu matumizi mabaya ya fedha, inawezekana kabisa lengo la shambulio hilo ni kumwondoa duniani mhasibu huyo ili kuondoa ushahidi wa hali hiyo,” alisema ofisa huyo wa juu serikalini.

Jitihada za gazeti hili kuwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Alfred Tibaigana ili kupata taarifa zaidi kuhusu suala hilo ziligonga mwamba jana.

Hili ni tukio la pili la maofisa wa juu wa serikali kuvamiwa majumbani mwao na kupigwa risasi, la kwanza likiwa ni lile lililomhusisha ofisa wa juu wa Wizara ya Afya ambaye aliuawa nyumbani kwake Segerea miaka ya hivi karibuni na watu ambao hawakuchukua kitu chochote.

Huko Rombo, mkoani Kilimanjaro nako, Jeshi la Polisi lililazimika kuwatia mbaroni maofisa wanne wa kampuni ya ujenzi ya Kichina ya SIETCO inayojenga barabara ya Tarakea, Rongai hadi Kamwanga kwa kiwango cha lami kwa tuhuma za kuvamia kituo cha polisi na kupiga askari wa kituo hicho.

Tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita, majira ya saa 3:00 asubuhi, ambako Wachina hao wakiwa kwenye kundi kubwa wanadaiwa kuvamia kituo cha polisi cha Tarakea na kuwashambulia askari waliokuwapo kituoni hapo.

Habari kutoka Tarakea zinadai kuwa, chanzo cha Wachina hao kutembeza mkong’oto kwa askari hao, ni hatua ya askari hao kuwazuia wasimpige deveva wa kampuni hiyo.

Chanzo cha habari kutoka Tarakea kimeeleza kuwa, dereva huyo aliyetambuliwa kwa jina moja la Michael, alikimbilia kituoni hapo kwa lengo la kujiokoa na kipigo cha Wachina hao wakimtuhumu kuiba mafuta kwenye magari ya mradi.

Wachina hao wakiwa na mapanga, walimvamia wakitaka kumpiga dereva huyo aliyekuwa akiendesha gari lililopewa namba 4 kwa kosa ambalo hadi sasa halijawekwa bayana.

Hata hivyo, dereva huyo alifanikiwa kuwaponyoka na akakimbilia katika kituo hicho cha polisi akiendesha gari analotumia.

Akiwa kituoni hapo kwa lengo la kuandikisha malalamiko yake dhidi ya Wachina hao, ghafla Wachina hao wakiwa katika kundi walikivamia kituo hicho na wakaanza kutembeza mkong’oto kwa kila aliyeonekana machoni mwao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Venance Tossi ambaye licha ya kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo, aliagiza Wachina wote waliohusika na tukio hilo wakamatwe mara moja na kufikishwa mahakamani.

Tukio hili ni la pili kutokea katika mradi huo. Mwanzoni mwa mwaka huu, maofisa wengine wa kampuni hiyo, walikamatwa na polisi wakituhumiwa kumpiga hadi kumjeruhi, mfanyakazi wao mmoja.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by washawasha)
    Rating
    Nchi hii sasa inaelekea kubaya iwapo wachina tu wakiwa na mapanga wanakimbiza kituo cha Polisi je wangekuja na bunduki ingekuwaje,tunaomba serikali irudishe hali ya amani nchini hapa kwa kututendea haki raia,yote haya yanatokana na serikali ya nchi ye2 mbovu hiyo kutuonea raia kisa wao wana miguvu,wachina hao inabidi wafikishwe mahakamani na kuhukumiwa kama wa2 wengine wanaofanya makosa,
    OMBI:
    Serikali lidhibitini jeshi la polisi kwa kuwaambia ni nini mipaka yao ya kazi la sivyo hatutokubali kuendelea kuonewa na jeshi hilo
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.